Baada ya kushindwa kufika Tanzania kwa ajili ya kuifundisha Yanga , kocha kutoka Burundi Cedric Kaze ametoa sababu kuu ya kwanini ameshindwa kufika Dar es Salaam kwa ajili ya kuifundisha Yanga.
Cedric Kaze amedai kuwa alikuwa na nia na alitamani kuifundisha Yanga ila matatizo ya kifamilia yamemfanya ashindwe kufikia matamanio yake kwa sababu akili yake isingekuwa katika klabu ya Yanga.
“Sababu ni kuwa tumepata matatizo kwenye familia. Siwezi kuweka wazi kwa sababu ni maisha binafsi .Na kazi ninayoenda kuifanya ni kazi kubwa ambayo inahitaji akili na roho yangu. Kwa hyo nikasema kuifundisha Yanga timu kubwa yenye mashabiki wengi wakati roho yangu haiko Yanga iko kwenye familia ni bora niache”. Alisema Cedric Kaze.
Cedric Kaze aliwapongeza viongozi wa Yanga kwa kumuonesha ushirikiano mkubwa tangu mwanzo mpaka muda wa mwisho ambapo ilishindikana yeye kuja Yanga.
“Niwapongeze Yanga tumekuwa tukisikilizana na kuelewana na viongozi vizuri ila kwa bahati mbaya dakika za mwisho tumeshindwa kuwa pamoja. Ni mipango ya Mungu ila napendelea mbeleni kuja kuitumikia Yanga”.
Alipoulizwa kama ameshindwa kuja Yanga kwa sababu ya kuogopa presha kubwa ya mashabiki , Cedric Kaze alisema kuwa presha ya mashabiki ni kitu kizuri kwa sababu kumpongeza hali na motisha.
“Sijaacha kujiunga na Yanga kwa sababu ya presha kubwa inayopatikana Yanga. Presha ya mashabiki ukiichukulia katika mlengo chanya huongeza motisha. Nimeacha kujiunga na Yanga kwa sababu kuna mwanafamilia anatakiwa kufanyiwa upasuaji.” Alifafanua Cedric Kaze.
Alipoulizwa ni wapi alipokuwa anafundisha kabla ya kuja Yanga , Cedric Kaze alidai kuwa, hakuwa na mkataba na timu yeyote baada ya mkataba wake na Barcelona kuisha.
“Sikuwa na timu yoyote kwa sababu mkataba wangu na Barcelona uliisha. Nilikuwa nafundisha timu za vijana za Barcelona. Baada ya mkataba wangu kuisha sikutaka kuongeza mkataba kwa sababu nilitaka nije ukanda wa Afrika Mashariki ili nifundishe mpira”- alimalizia Cedric Kaze.