Yanga watashuka dimbani leo Jumamosi saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki katika fainali ya mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Algier, tayari katika mchezo wa kwanza Yanga walipoteza nyumbani.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza wakiwa Benjamin Mkapa Yanga walipoteza kwa mabao mawili kwa moja na hivyo wanakibarua chakupindua matokeo ili kutimiza ndoto yakutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Kutokana na kiwango kizuri na matokeo mazuri waliyoyapata Yanga katika michezo ya ugenini msimu huu katika michuano hiyo bado inawapa matumaini mashabiki wa Yanga kuelekea mchezo huo.
Katika msimu huu Yanga imecheza michezo sita ugenini wakishinda michezo minne, wakisare mmoja na kupoteza mchezo mmoja. Walianza kushinda dhdi ya Club Africain Tunisia halafu wakawafunga TP Mazembe Congo na kuibuka na ushindi mbele ya Rivers United na Marumo Gallants katika robo na nusu fainali.
Yanga msimu huu wamepoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya US Monastir Tunisia na sare dhidi ya Real Bamako ya Mali. Na hiki ndio kinawapa jeuri Wananchi kuweza kutimiza ndoto zao.
Kocha wa Yanga Nasraddine Nabi tayari ameshawaona Algier katika mchezo wa awali na hivyo tayari anajua walikosea wapi katika mchezo wa awali na hivyo anajua chakufanya kuelekea mchezo huo wapili. Mbinu za Profesa Nabi leo zinahitajika na ndio zitaamua leo Yanga inapata matokeo gani.
USM Algier wamekua wakitumia mawinga wake kushambulia wakipitia pembeni wakiamini katika kasi za mawinga wao, pia wamekua wakipenda kuanzisha mashambulizi yao kuanzia chini wakiwa na walinzi wazuri wa kati wenye uwezo wa kuchezea mpira bila wasiwasi.
Nabi pia anapaswa kuendelea kutafuta njia sahihi za kuwadhibiti Algier katika mipira iliyokufa, Waarabu hawa ni dhahiri wataendelea kutumia mipira ya kona na adhabu kuendelea kuzalisha magoli yao kutokana na udhaifu wa Yanga katika kucheza mipira hiyo.
Kikosi cha Yanga huenda kikaanza hivi, Djigui Diara, Dickson Job, Lomalisa Mutambala, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Yanick Bangala, Mudathir Yahya, Jesus Moloko, Fiston Mayele, Sure Boy na Kenedy Musonda. Ama kwa hakika ni kikosi kitakachowafanya Wananchi waishi ndoto zao.