Sambaza....

Walatini wana msemo wao’ Octa Non Verba’ yaani maneno kidogo vitendo zaidi

Moja ya Kocha ambaye anapenda vitendo vizungumze kuliko kubwabwaja mineno ni huyu wa Geita Fred Felix Minziro “Baba Isaya”.

Yawezekana ndie kocha ‘underated’ kwenye familia ya mpira kwa maana ya kutokupewa thamani halisi anayostahili kuanzia kwa waajiri wake na vyombo vya habari ikiwemo wadau na mashabiki wa mchezo huo.

Binafsi naona hapewi thamani ambayo angeweza kupewa kocha wa kigeni kutengenezewa ‘publicity’ zaidi ya hii aliyonayo sasa hasa baada ya kuifikisha Geita Gold hapa ilipo siyo jambo dogo.

Kwa sasa Geita inauhakika wa kumaliza kwenye nafasi ya nne kwa maana yeyote iliyopo kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

Alama 45 alizonazo kwenye msimamo wa ligi unamfanya kutofikiwa na timu yeyote ile huku juu yake kukiwa na Azam 46 Simba 60 na Yanga 71.

Geita haiwezi kuzifikia Simba au Yanga kwa alama walizonazo na kwa lugha nyingine wameshapata uwakilishi wa kimataifa.

Shughuli ipo kwenye nafasi ya tatu na ya nne ambayo inawaniwa na Azam na wao Geita ya Minziro ili kuwa na uhakika wa kuwakilisha kimataifa.

Kwa kuwa ukifanikiwa kuingia kwenye 3 bora unakuwa na uhakika wa 100% kuwakilisha kimataifa bila kujalisha matokeo ya kombe la Azam sport federation cup liende kwa nani.

Kinyume na hapo ukiwa kwenye nafasi ya 4 utalazimika kusubiri majaliwa ya Yanga kutwaa kombe la FA ili kuruhusu timu yeye nafasi hiyo kufuzu kimataifa kwa kuwa Wananchi tayari watakuwa na nafasi moja.

Haikuwa jambo jepesi kwa Geita kuchukua nafasi hiyo kwa kupitia Kocha mzawa Fred Felix Minziro na kikosi chake kilichosheheni wachezaji wazawa watupu.

Hapa ni lazima benchi la ufundi linaloongozwa na Minziro akisaidiwa na Mathias Wandiba pamoja na Waziri Mahadhi Mandieta wapongezwe kwa dhati kabisa.

Wametoa somo kubwa kwenye soka letu na hii inamaana kama wakipewa nafasi kutengeneza timu msimu ujao wanaweza wakasumbua zaidi.

Hongera sana Kocha Minziro na benchi lenu la ufundi wachezaji na uongozi hakika mmetoa somo kubwa kwenye ushiriki wenu wa ligi kuu.

Sambaza....