Kuelekea mchezo wao wa marejeano wa Caf Confederation Cup dhidi ya KCCA FC ya Uganda kesho Jumamosi, nahodha wa Mtibwa Sugar FC, Shaaban Nditti amekiri watalazimika kucheza ‘kufa na kupona’ ili kupindua matokeo ya 3-0 na kufuzu kwa hatua ya mwisho kuwania nafasi ya kufuzu kwa hatua ya makundi.
Kikosi hicho cha kocha Zubery Katwila kulichapwa mabao 3-0 wiki iliyopita huko Kampala, Uganda na ili kifanikiwe kuvuka raundi hii ya kwanza ni lazima washinde tofauti ya magoli manne au 3-0 na kujaribu kufuzu kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.
” Tutajaribu kila tuwezalo ili kuvuka hatua hii, lakini kipigo cha wiki iliyopita kukikuwa kikubwa sana kwetu.” anaanza kusema Nditti ambaye ni mchezaji mkongwe zaidi katika timu hiyo ya Turiano, Morogoro.
” Tuna kukosi chenye wachezaji wachanga na wale wenye uzoefu. Tuna vipaji vya kutosha na makocha wenye uwezo wa kutusaidia kuvuka hatua hii.”
Mtibwa iliruhusu magoli matatu baada ya kuwabana Waganda hao kwa saa nzima Jumamosi iliyopita.
“Lazima tuwe makini. Tulicheza vizuri kwa muda mwingi wa mchezo wa awali lakini baadaye tulianza kupoteza mwelekeo na kuruhusu magoli ya harakaharaka. “anasema Nditti na kuongeza.
” Tunapaswa kuwa makini katika ulinzi na kuhakikisha tunatumia kila nafasi tunayotengeneza kufunga magoli. Tukumbuke hatuhitaji ushindi tu, bali ushindi utakaotusaidia kuvuka hatua hii.”