Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa Ligi kuu nchini England lazima utakua unalijua/unalisikia jina hili ONYINYE WILFRED NDIDI. Huyu ni kiungo mkabaji anayekipiga kunako klabu ya Lecester City pale England huku akikichafua kinoma eneo la kiungo wa ulinzi.
Jamaa huyu alizaliwa tarehe 16 Disemba 1996, ni mtoto wa kwanza na kiume pekee kati ya watoto watatu wa Soja mmoja pale Lagos Nigeria. Wakati kiungo huyu anakua, Baba yake hakutaka kabisa acheze mpira kwani alihitaji kijana arithi mikoba yake ya kuwa Mwanajeshi.
Ndidi aliona sio mpango kuwa Mwanajeshi kwani aliupenda sana mpira wa miguu , kiasi kwamba akawa anakosana mara kwa mara na baba yake. Mambo yaliendelea kuwa hivyo mpaka mwaka 2013 ambapo Ndidi aliitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Nigeria kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, ambao walishiriki michuano ya Mataifa ya Afrika kwa umri huo na kijana huyo alicheza kwa kiwango kizuri katika eneo la dimba.
Baada ya hapo mzee wake aliona isiwe tabu ni vyema akatoa baraka zake zote kwa Mwanae na kumruhusu kucheza mpira rasmi huku akimsaidia ili aweze kutimiza ndoto zake.
Baraka za mzee wake ndio kitu alichokua akisubiri tu kwani baada ya hapo mambo yalimnyookea, kupitia mashindano hayo ya ‘Africa U17 Championship’ wasaka vipaji kutoka Ubelgiji walimuona na kuvutiwa nae hivyo kupelekea kujiunga na KRC Genk! Akiwa Genk pia alikutana na Mbwana Sammata.
Unajua nini kilifuata akiwa Genk? Ilimchukua misimu miwili tu 2015/16-2016-17, kuonesha kuwa tayari mguu wake umefika ‘Level’ za kukipiga kunako ligi kubwa Duniani (England) na kumwaga wino pale Leicester city mwaka 2017, ambako anapiga mali mpaka leo.
Jamaa akiwa Dimbani unaziona kabisa chembe chembe za ujeshi ndani yake, anakaba mnoo, anawafanya watu wanaomzunguka kama James Maddison na Jimmy Vardy kuuona mpira kitu rahisi.
Hayo yote yalianzia pale alipokacha mpango wa baba yake ‘kuwa mwanajeshi’ na kujikita kwenye soka.
Ndidi ana umri wa miaka 23, na bado yuko fiti hivyo ni hazina kwa timu yake ya Taifa Nigeria “Super Eagles” na klabu yake pia ni mchezaji muhimu kikosini. Lakini pia ni bidhaa pendwa sokoni huku tetesi tayari zimeanza kuibuka aanatakiwa na klabu kubwa nchini Uingereza. Tusubiri tuone nini kitatokea.