Sambaza....

Tuko kwenye dunia ya kibiashara, dunia àmbayo imejaa ushindani mkubwa ndani yake. Ushindani ambao unasababishwa na taasisi nyingi kila siku kufikiria namna ambavyo zinaweza kufanya uzalishaji wa kiwango bora.

Uzalishaji bora ni kitu cha msingi sana kwenye maisha. Na ndiyo silaha ya kwanza kwenye ushindani wa kibiashara.

Unaweza ukawa na silaha nyingi ambazo unaweza kuzitumia kujivunia kwenye ushindani wa kibiashara lakini silaha ya kwanza ni uzalishaji bora wa bidhaa zako.

Kwa bahati mbaya sana sisi Wa Afrika tunaamini katika wingi wa bidhaa na siyo kwenye ubora wa bidhaa husika. Na hii inatokana na kwamba huwa tunaogopa sana gharama za kitu ambacho kipo katika hali ya ubora.

Na kwa bahati mbaya zaidi hatujawahi kuwaza kuwa mpira ni biashara. Akili zetu zinaamini kuwa mpira ni kujitoa kwa moyo.

Hatujawahi kuweka akili za kibiashara kwenye mpira ndiyo maana ni ngumu kwetu sisi kupata kitu ambacho ni bora kwenye mchezo huu unaopendwa na watu wengi.

Siku zote matokeo bora au uzalishaji wa bidhaa bora katika mpira wa miguu unatokana na timu husika kuwa na wachezaji bora ndani ya kikosi.

Wachezaji bora ambao wanapata huduma bora, huduma ambazo zitaongeza morali ya wao kucheza katika kiwango bora.

Mchezaji anapokuwa anapata huduma bora, kichwani mwake hubaki na deni la kulipa. Deni ambalo hutakiwa kulilipa uwanjani.

Hapo ndipo dhana ya mpira biashara inapoanzia. Mwajili hutumia pesa nyingi kutengeneza mazingira bora kwa mwajiliwa kufanya kazi kwa amani.

Huyu mwajiliwa anafamilia ambayo inamtegemea , na kipaji chake ndicho ambacho kinatakiwa kutumika ili aingize kipato kwa ajili ya kuilisha familia yake.

Huyu mwajiliwa ambaye ni mchezaji umri wake wa kucheza kwa kiwango kikubwa ni mchache sana , hivo lazima atumie wakati ambao yuko katika kiwango cha juu kuingiza pesa ambayo itamsaidia kwa baadaye.

Maisha ya mpira wa miguu ni mafupi sana. Wachezaji wengi huzeeka wakiwa na umri wa miaka kuanzia 30. Hapo ndipo nguvu za mchezaji husika huanza kupungua.

Ni nadra sana yeye kucheza katika kiwango cha juu kama ambavyo alivyokuwa na umri wa miaka 25. Kwa hiyo anapofikisha umri wa miaka 30 hukaribisha kustaafu.

Anapostaafu anatakiwa kuishi maisha ambayo aliyachuma wakati anacheza mpira wa miguu. Hapo ndipo huwa mwanzo wetu kuwananga wachezaji.

Vinywa vyetu huinuka juu kwa kuwasema vibaya. Utasikia huyu akidai kuwa wachezaji wa bongo hawajielewi kwa kile ambacho walishindwa kupata hata pesa kidogo wakati wanacheza mpira wa miguu.

Wakati huu wengi wanaweza wakawa katika upande wa Mwinyi Zahera. Na wanaweza wakawa wanampa nguvu kubwa sana baada ya yeye kutomtaka Beno katika kikosi chake.

Na kuna mwana Yanga atasikika akisema kuwa hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya Klabu. Kitu ambacho ni kweli, lakini hawawezi kutazama upande wa pili kwa mchezaji.

Watakuja kuutazama huo upande wakati Beno Kakolanya kastaafu mpira akiwa hana kibanda cha kupumzisha ubavu wake usiku.

Na hapo wataanza kumnanga kweli!, watamsema sana na watamwiita mtu ambaye hajielewi kwa sababu tu hakuweza kupata hata shilingi kadhaa wakati anacheza mpira.

Hapa ndipo unafiki wa BINADAMU unapoonekana. Mimi sitaki kuwa mnafiki kwenye hili na nimetokea kumwelewa Beno Kakolanya kuliko Mwinyi Zahera.

Namwelewa sana Beno kwenye hili. Namwelewa kuwa ana familia kubwa kwa sasa inamtegemea sana. Namwelewa mno!.

Namwelewa Beno Kakolanya kuwa anaihofia kesho yake. Najua kwa sasa anajiuliza sana Kesho yake itakuwaje na anaihofia sana.

Anahofia kuishi maisha ya kuomba omba hapo kesho ndiyo maana anadai haki ya jasho lake wakati huu akiwa na nguvu ili aitengeneze kesho yake iliyo bora.

Namwelewa sana Beno Kakolanya kwa sababu anaipa ujumbe Yanga kuwa inatakiwa kutimiza majukumu yake kwanza ipasavyo kabla ya mchezaji kutimiza hayo majukumu.

Namuelewa sana Beno Kakolanya kwa sababu anajaribu kutukumbusha kuwa tupo kwenye dunia ambayo siyo ujamaa.

Dunia ya kibepari, biashara ni nguzo muhimu sana kwenye dunia hii. Dunia ambayo kila kitu lazima kifanyike kwa njia ya kibiashara.

Beno Kakolanya anawakumbusha Yanga kuwa wanatakiwa kujiendesha kibiashara na siyo kama ambavyo inajiendesha kwa sasa.

Namuelewa sana Beno kwa sababu anatuambia kwa pamoja kuwa kwenye dunia hii ya kiushindani lazima taasisi ishiriki katika kutengeneza bidhaa bora na bidhaa bora hupatikana baada ya kuwapa huduma bora wafanyakazi wa taasisi.

Sambaza....