Sambaza....

Kupangwa na timu kutoka Ushelisheli ilikuwa furaha kubwa kwa Yanga kwa sababu furaha yao waliitengeneza kutokana na historia yao ya nyuma.

Historia ya Yanga ilikuwa imeshiba dhidi ya hivi vilabu vya visiwani kama Comoro, Ushelisheli

Haikuwa jambo la kushangaza kusikia Yanga wameitoa timu kutoka katika visiwa hivi kwa jumla ya magoli mengi.

Kwao wao walikuwa wanajipigia wapendavyo, hakuna ambaye angeweza kuwazuia au hata kuwashauri kupunguza uzito wa vipigo kwa hizi timu.

Jambo hili liliwafanya wapate viburi kwa kiasi kikubwa kila walipoona wanakutana na timu kutoka hizi sehemu.

Hata walipokutana na St. Louis walijua kabisa jana inaweza ikawa na taswira ya leo, kitu ambacho kilikuwa tofauti sana.

Ushindani waliokutana nao haukuwa ushindani ambao umezoeleka kwa kipindi cha nyuma, hakukuwepo na urahisi tena kwa Yanga kwenye mechi hii.

Hadithi ya Yanga kuzitoa timu za ukanda huo kwa jumla ya magoli 2-1 ilikuwa hadithi ambayo ilikuwa haijazoeleka katika masikio na macho ya mashabiki wa Yanga.

Siku za nyuma hadithi yao ilipambwa na majigambo ya kuzitoa timu za ukanda huu kwa jumla ya magoli 7-1, 5-1 ! , n.k

Hata walipovuka kwenda hatua ya awali, kazi ilionekana rahisi sana kwa Yanga kwa sababu walikuwa wanaenda kukutana na timu ya Township Rollers kutoka Botswana.

Kwa macho ya kawaida ilikuwa mechi rahisi sana kwao kwa sababu Township Rollers ilikuwa inatoka kwenye nchi ambayo kiwango chake cha mpira siyo kikubwa sana.

Hivo wengi walitegemea Yanga ingeweza kufanya vizuri na kuwatoa hawa watu, ƙlakini hadithi ikasomeka kinyume na Yanga ikatolewa katika mashindano haya na kushushwa kwenye kombe la shirikisho barani Afrika.

Sehemu ambayo anaenda kukutana na timu ambayo inaonekana pia kama timu isiyotisha sana kwa sababu imetokea katika nchi ambayo kiwango chake cha soka barani Afrika siyo kikubwa sana.

Hadithi ya Yanga msimu huu inakuwa ile ile tangu mwanzo mpaka sasa hivi inapofika hatua hii.

Tangu mwanzo Yanga inaonekana imekutana na timu ambazo siyo tishio kwa kiasi kikubwa kila zikitamkika midomoni mwa watu kwa sababu hata historia zao huko nyuma hazikuwa na historia ya kutisha.

Yanga waliona ukawaida ƴusio wa kawaida kila walipokuwa wanakutana na hizi timu. Ndiyo maana walicheza kawaida kwa sababu walijua wanaenda kukutana na timu za kawaida.

Hakukuwepo na njaa kwenye miguu ya wachezaji wa Yanga kitu kilichopelekea hata kushindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani katika michezo yote miwili iliyochezwa hapa nyumbani.

Nafasi nyingi za wazi walikosa, nidhamu ya matumizi ya nafasi ilikuwa haipo ndani ya wachezaji wa Yanga.

Mchezo wa kwanza dhidi ya St.Louis walipoteza mpaka penalti, wakashinda ushindi mwembamba, ushindi ambao haukuwapa asilimia kubwa ya kupita. Hata walipoenda kwenye uwanja wa ugenini mechi ikaonekana ngumu kwao pia.

Ugumu huu waliutengeneza pia kwenye mechi dhidi ya Township Rollers waliyocheza hapa nyumbani. Hadithi ilikuwa ile ile, Yanga walipoteza nafasi nyingi hapa nyumbani , hawakuwa na nidhamu ya matumizi ya nafasi katika uwanja wao wa nyumbani, kitu kilichopelekea mechi iishe hapa nyumbani.

Wolaita Dicha

Tatizo la kwanza la Yanga katika mashindano ya kimataifa msimu huu ni kutomheshimu mpinzani wao kwa kila hatua ambayo walikuwa wanaipiga.

Hali ambayo ilisababisha wao kujiamini sana , kujiamini kwao kuliwaondolea umakini. Hii ilikuwa rahisi kwao kukosa nidhamu ya matumizi ya nafasi walizokuwa wanazipata.

Hivo nidhamu ya matumizi ya nafasi kiwe kitu cha msingi katika mchezo huu dhidi ya Wolaita Dicha ya Ethiopia. Wasiruhusu ile hali ya kujiamini sana ambayo itawaondelea hata umakini ndani yao.

Sambaza....