Sambaza....

Mkurugenzi wa klabu ya soka ya Real Madrid Emilo Butragueno amesema klabu hiyo inaridhika na kazi ya kocha Santiago Solari baada ya kushinda mechi nne mfululizo kwa mara ya kwanza toka kuanza kwa msimu baada ya kuichapa Celta Vigo jana Jumapili.

Butragueno amesema ushindi wa jana wa mabao 4-2 dhidi ya Celta Vigo unaifanya klabu hiyo kuanza kurejea taratibu katika ushindani na kujiamini baada ya kutokuwepo toka kuanza kwa msimu, na mchezo wa ana ulikuwa ni wa mwisho katika mkataba wa kocha Solari ambaye alipewa majuma mawili kuiongoza klabu hiyo baada ya kutimuliwa kocha Julen Lopetegui Argote.

“Amefanya kazi nzuri, amefika katika muda sahihi na kufikia mafanikio makubwa, ukiondoa michezo yote ambayo ameiongoza Real Madrid mchezo dhidi ya Celta Vigo ulikuwa mgumu zaidi lakini ameweza, tunafuraha kwa namna mambo yameenda,” amesema Butragueno.

Licha ya kumsifia kote huko lakini Butragueno alishindwa kuthibitisha kama Real Madrid wapo tayari kumuachia mazima kocha huyo wa timu ya Vijana kibarua hicho kigumu kwa timu kubwa kama hiyo.

“Tutaona, mara nyingi sipendi kufikiria mbali sana, muhimu zaidi ni kufanya maamuzi ambayo yatakuwa mazuri kwa klabu, hakuna kitu muhimu zaidi ya hicho,” amesema.

Toka kuwasiri kwa kocha huyo Real Madrid wamefanikiwa kufunga mabao 15 huku wakipunguza wigo wa alama 4 kutoka kwa vinara Barcelona kwenye ligi kuu soka nchini Uhispania.

Sambaza....