Baada ya Aston Villa kuweka rekodi ya uhamisho na kumsajili mshambuliaji Ollie Watkins kutoka Brendford kwa ada ya £28milioni ni wazi nafasi ya Mbwana Samatta kuanza katika kikosi cha kwanza ilikua finyu.
Nahodha huyo wa Timu ya Taifa ya Tanzania hakuonekana kukataa tamaa walaa kushtushwa na usajili huo wa nyota huyo eneo lake, badala yake aliendelea kuweka akili na nguvu katika mazoezi ya mwanzoni mwa msimu na kikosi cha Villa.
Lakini habari mbaya zaidi kwa Mbwana Samatta sasa ni usajili wa Betrand Traore mshambuliaji nyota kutoka Olympic Lyon ambapo tetesi zinasema dili lake limeshakamilika tayari akiwa ameshafanya vipimo vya afya huenda ukakamilika ndani ya masaa 48 yajayo akisubiri visa ya kuingia nchini Uingereza.
Traore mchezaji wa zamani wa Chelsea anakwenda kuungana tena na kocha John Terry. Wawili hawa walikutana Chelsea kama wachezaji lakini sasa Traore atakwenda kukutana na kocha msaidizi John Terry ambae anamfahamu vizuri.
Kiasi cha £17millioni kinatajwa kama dau la kung’oa Traore na kuhamia Villa Park. Usajili huu ukikamilika ni wazi sasa Samatta atakua mshambuliaji namba tatu mbele ya machaguo ya mwalimu Dean Smith na msaidizi wake John Terry. Ollie Watkins, Betrand Traore na Keinan Davies wote hawa wapo katika orodha ya eneo la ushambuliaji la Aston Villa.
Hapana shaka njia ya Samatta kuondoka Villa Park imekua nyeupe, ni yeye mwenyewe kuchagua kusugua benchi ama kwenda kutafuta malisho mahala pengine.