Kuna mengi sana hutokea kwenye maisha tofauti na mategemeo yetu. Maumivu huwa vazi letu kipindi tunapopata matokeo yaliyotofauti na mategemeo yetu.
Kuna vingi huvitegemea na kuvisubiri kwa hamu vitokee ili vikamilishe furaha yetu lakini muda huja na uhalisia ambao hugeuka kuwa ukweli.
Uhalisia ambao huonekana mchungu, uchungu ambao hugeuka kuwa ukatili lakini cha kusikitisha vitu vyote huonekana mbele ya mboni za macho yako.
Utaumia, utalia na kukosa raha lakini ukweli ni kwamba unachokipitia ndiyo uhalisia , uhalisi ambao huja wakati sahihi.
Ndiyo maana tukafundishwa tujifunze kupokea kuliko kutegemea ( learn to accept than to expect).
Tulitegemea furaha kwa Arsene Wenger msimu huu, tulitegemea ataondoka akiwa na tabasamu katika uso wake.
Mategemeo haya makubwa yaliuvaa moyo wake. Moyo wake uliamini ataondoka Arsenal akiwa na furaha kubwa sana tofauti na alivyokuja.
Hata siku anatangaza kuachana na Arsenal wachezaji wa Arsenal walimwahidi kupigana kwa ajili ya furaha yake, kwa bahati mbaya wakasahau kila mwanadamu anajukumu la kutengeneza furaha yake mwenyewe.
Hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa Arsene Wenger kujitengenezea njia yenye mimba ya huzuni.
Huzuni ambayo kwa sasa imemvaa mwili mzima peke yake, hakuna wa kumuonea huruma tena kwa kiasi kikubwa kwa sababu awali aliambiwa akashupaza shingo.
Hakutaka kusikia msimu jana alipoambiwa apumzike kwa amani baada ya kupata kombe la FA.
Imani yake ilimpa nguvu kuwa anaweza kupambana msimu huu kuchukua kombe la ligi kuu ya England.
Hakujisumbua kumwaangalia Pep Guardiola alivyotoa pesa nyingi kwa ajili ya mabeki.
Hakuona kabisa umuhimu wa ujenzi wa ukuta imara wa kujilinda.
Kitu alichokiamini yeye ndicho hicho atakisimamia, hakutaka ushauri. Hakuamini katika kuendesha timu kisasa kwa kujipa tumaini anaweza kupitia njia alizopitia 2003/2004 katika dunia hii ambayo kipa ananunuliwa kwa paundi 30M.
Ndiyo maana hata alipoambia aletewe Director of Football katika timu yake alihoji huyu ni nani?, ataisaidia nini timu ?.
Hakutaka hata siku moja mgawanyo wa majukumu ya kiufundi uwepo ndani ya timu. Alikiamini kichwa chake, akayatukuza macho yake na akaishujudia akili yake lakini akasahau kitu kimoja kuliambia sikio lisikie.
Hakutaka kulipa ruhusa sikio lake kuwa wazi, alitumia muda mwingi sana kuliziba kwa pamba nyingi sana ili mradi tu asisikie chochote kutoka kwa watu waliokuwa wamemzunguka.
Hata ilipotokea mtu kachomoa pamba sikio mwake na kumwambia kitu, jeuri ilikuwa zawadi tosha kutoka kwa Arsene Wenger.
Ungemwambia kipi Arsene Wenger akusikie kuhusu safu yake dhaifu ya ulinzi iliyodumu kwa miaka 12 mfululizo?
Ungemkumbusha kipi akumbuke kuwa tangu mwaka 2006 hajafanikiwa kutengeneza ukuta imara ndani ya Arsenal? Ukuta uliomfikisha fainali ya UEFA bila kufungwa hata goli moja kuanzia mechi za makundi akaja kufungwa fainali?
Kipi angesikia na kukuelewa kipindi ambacho ungetumia muda wako unamkumbusha kuwa tangu mwaka 2006 kombe alilochukua lilikuwa kombe la FA pekee?
Alibaki kuamini njia zake, alikiamini kikosi chake. Alimwamini Ramsey ndiye kiungo bora duniani kwa sasa.
Majeruhi ya Dany Welbeck yalivumilika kwa mzee Arsene Wenger kwa sababu aliamini Dany Welbeck yupo juu ya kina Luiz Suarez.
Hili ndilo daraja alilokuwa anatembea nalo, daraja ambalo lilikuwa linamwaminisha kuwa anaweza akambadili mchezaji wa kawaida kuwa mchezaji mkubwa.
Aliishi kwenye dunia ya kina Henry katika ulimwengu ambao kina Pep Guardiola hawaamini tena kupitia La Masia.
Alibaki Arsene Wenger tu na imani yake, imani ya kumwamini Chambers na Holding kumpa kombe kubwa.
Hapa ndipo mwanzo wake wa kushindwa kupata furaha kwenye mwisho wa safari yake ulipoanzia.
Leo hii anaondoka kama alivyokuja, hana kikombe cha kumfariji, huzuni , majonzi yamemvaa usoni.
Hana tena mfariji kipindi hiki kwa sababu waliokuwa wanamshauri hakutaka kuwasikiliza na aliwaona hawafai, leo hii wamemwacha peke yake kwenye dunia ya peke yake.
Dunia ya huzuni kubwa, dunia ya upweke mkubwa , hana shabiki, kiongozi, mchezaji hata mke wa kumfariji tena. Anatembea mwenyewe kwenye shamba alilopanda mbigili hakuna wa kumletea viatu vya kustiri unyayo wake.