Sambaza....

Kuelekea Dabi namba tano kwa ubora Barani Afrika kati ya Simba Sc na Yanga msemaji wa Klabu ya Simba Ahmed Ally amesema hawapo tayari kwa vyovyote vile kupoteza mchezo huo.

Kuelekea mchezo huo utakaopigwa April 16 Jumapili hii mbele ya Waandishi wa habari msemaji wa klabu ya Simba Ahmed Ally amesema wanaitaka mechi kwelikweli.

 

“Mechi hii Wanasimba tunaitaka kwelikweli, mechi hii lazima tuambiane ukweli wana Simba tuna hamu nayo kwelikweli, yaani April 16 tunaitaka haswa. Mwanasimba nunua tiketi yako mapema uweze kuingia uwanjani,” alisema na kuongeza

“Sisi kama uongozi tayari tumefanya majukumu yetu kuelekea mchezo huo na wachezaji wakiamua hakuna lolote litakaloshindikana na kuweza kupata ushindi ambao tumeukosa kwa muda mrefu mbele ya Yanga. Itakua haina maana kumfunga Horoya kutoka Guinea huko mabao saba halafu tushindwe kumfunga Yanga wa hapahapa,” Ahmed Ally

Msemaji huyo pia ameonyesha tayari Simba wameshaukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara lakini hawapo tayari na hawatakubali kufanywa kuwa ngazi ya Yanga katika kuwapa ubingwa.

“Itakua ni fedheha kubwa sana kwa Yanga kutufunga na kutangazia ubingwa kwetu,  utakua ni udhalilishaji mkubwa kwetu kwa Yanga kutangazia ubingwa kwetu na itakua ni aibu ya karne kama Yanga watatangazia ubingwa mgongoni kwetu.

Tutadondoka na kushindwa kuchukua ubingwa lakini sio kufungwa na kutangaziwa ubingwa mbele yetu. Narudia tena hatupo tayari kuwa ngazi ya Yanga kwenye kutagazia ubingwa,” alisema Ahmed Ally. 

Simba watakua nyumbani wakiikaribisha Yanga katika Dimba la Benjamin Mkapa saa kumi na moja jioni siku ya Jumapili. Katika mchezo wa raundi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao moja kwa moja.

 

Sambaza....