Baada ya Bernard Morrison kuonekana kwenye viwanja vya mazoezi akiwa na timu yake ya Yanga , maswali mengi yalizidi kuibuka kwa wadau wa soka nchini . Moja ya swali kubwa ni kama Yanga walimsamehe Bernard Morrison ambaye walikuwa wamemsimamisha kutokana na utovu wa nidhamu.
Mtandao huu wa kandanda.co.tz uliamua kumtafuta Afisa Habari wa Yanga , Hassan Bumbuli kutolea ufafanuzi suala hili la Bernard Morrison kuonekana mazoezini na yeye kutoenda Mara kwa ajili ya mechi dhidi ya Biashara United ya Mara.
Hassan Bumbuli amedai kuwa mpaka sasa hivi viongozi wa Yanga hawajui na hawatambui kama Bernard Morrison amejiunga kwenye uwanja wa mazoezi wa Yanga pamoja na picha zake kuonekana akiwa kwenye mazoezi na Yanga.
“Uongozi wa Yanga hautambui kujiunga kwa mazoezi kwa winga wa Klabu hiyo Benard Morrison ambaye bado ana kesi na Klabu hiyo kuhusu kutoutambua mkataba mpya wa miaka miwili”. Amedai Afisa habari huyo wa Yanga.
Bumbuli amedai kuwa Morrison hakuwepo kwenye mipango ya Timu kwa mechi za Kanda ya ziwa na mechi nyinginezo Kutokana na matatizo aliyonayo na Uongozi. Hata kujiunga na mazoezi ya Timu uongozi haukuwa na taarifa zaidi ya kuona kocha mkuu Luc Aymael akisema amemsamehe.