Sambaza....

Klabu ya soka ya AS Monaco ya nchini Ufaransa imemtangaza mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo na vilabu vya Arsenal na Barcelona Thierry Henry kuwa kocha wao mkuu hadi Juni mwaka 2021.

Henry ambaye alikuwa kocha msaidizi wa Ubeligiji katika fainali za kombe la Dunia anachukua nafasi ya Leonardo Jardim aliyetimuliwa kazi Alhamis kutokana na matokeo mabovu timu hiyo imekuwa ikiyapata kwa siku za hivi karibuni.

Henry mwenye umri wa miaka 41 anarejea tena Monaco alipoanza safari ya soka ambapo akiwa hapo aliisaidia timu hiyo kutwaa taji la ligi mwaka 1997 na sasa akiwa kama kocha anatazamiwa kwanza kuinasua timu hiyo mkiani ikiwa katika nafasi ya 18 ikiwa imeshacheza michezo tisa.

“Ni kama hatima yangu kuanza kila kitu katika klabu hii, na sasa naanza safari yangu ya ukocha hapa, Monaco itabaki kuwa katika moyo wangu, ninashauku kubwa kupewa majukumu haya, lakini kazi nzito inatakiwa kuanza” amesema Henry ambaye pia aliwahi kuchezea Juventus na New York Bulls.

Awali kabla ya kupewa kibarua hicho alihusishwa sana na klabu ya Aston Villa ambapo amekiri akisema kwamba ilikuwa ni kazi yenye ushawishi mkubwa lakini kwa sasa anafuraha kurejea Monaco.

Monaco kumtangaza Henry kama mrithi wa Jardim

Henry mwenye rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Arsenal akiwa na mabao 228 atakuwa na kibarua kizito atakapowakabili Strasbourg katika mchezo wake wa kwanza kutafuta ushindi wa pili katika ligi ndani ya michezo 9, kabla ya kwenda kuumana na Club Brugge kwenye michuano ya ligi ya Mabingwa.

Sambaza....