Jioni nilikuwa nautamaduni wa kwenda kucheza mpira kila nikitoka shule. Utamaduni ambao ulikuwa unawaudhi sana wazazi. Kwao wao hawakuona umuhimu wa mimi kucheza mpira, kwa sababu hawakuona faida yoyote ya mpira.
Tangu wakiwa watoto waliaminishwa mpira ni starehe, ni mchezo wa kujifurahisha tu na siyo biashara. Hawakuwa na imani kabisa kuwa mpira unaweza ukamtengeneza mtu akawa tajiri mkubwa sana duniani. Ilikuwa ngumu sana kuwaaminisha kwenye hili. Na ni kweli utaanzaje kuwaaminisha kuwa mpira unalipa wakati tangu utoto wao mpaka uzee umewafika hawajawahi kushuhudia hata kijana mmoja akifanikiwa kupitia mpira?
Hiki ni kitu kigumu sana na ilihitajika akili ya ziada sana kuondoa nadharia hii kwenye akili zao, nadharia ambayo ilijengwa pia na serikali yetu. Serikali yetu iliwaaminisha wananchi wake kuwa mpira ni burudani, yani kwa kifupi michezo yote kwetu iilikuwa na bado inatambulika kuwa ni ridhaa, siyo kazi kama kazi nyingine ambazo jamii inaweza kumtazama mtu na kumuona kuwa huyu anaenda ofisini.
Jamii zetu zimefanywa ziamini kazi ni zile ambazo mtu anaenda ofisini akiwa na nguo zake nadhifu, huwezi kuanza kuilaumu jamii yetu kwa sababu hiki kitu kimejengeka kwa kiasi kikubwa. Ndiyo maana fimbo zilikuwa rafiki wa makalio yangu kila nilipokuwa natoka kucheza mpira na watoto wenzangu.
Mzee hakutaka kusikia habari za mimi kwenda kucheza mpira kila nilipokuwa natoka shule, akili yake ilitaka kuniona mimi nikishika daftari kwa ajili ya kujisomea kila nikitoka shule, aliona mpira ni sehemu kubwa ya mimi kujifunza uhuni.
Mzee wangu hakutaka hata siku moja niharibikiwe na chochote kile, alikuwa anayapenda sana maisha yangu ndiyo maana alisimama kuwa kiongozi imara kwenye maisha yangu. Alinipa nasaha nyingi sana za kufundisha ambazo mpaka leo zinaishi kwenye kumbukumbu zangu.
Moja ya nasaha bora kuwahi kunipa ni hii ambayo kabla hajanipa alinichapa sana. Alinichapa mno!, kichapo ambacho hata yeye alijihisi amekosea kunichapa vile!, mbele ya macho yake niliiona huruma yake kwangu!, na nafsi yake ilizungumza wazi kuwa amekosea sana lakini kama mtu mzima hakutaka kuniomba samahani.
Ni ngumu kwa mtu mzima kujishusha kwa mtoto wake na kumuomba msamaha , hata kama ataomba msamaha basi ataomba kiutu uzima. Ndicho kitu ambacho mzee wangu alichokifanya. Hakutaka kusema nisamehe Kiyumbi. Hakutaka kabisa kukiri kuwa Kiyumbi nimekosea sana kukupiga hivo.
Hakutaka kuonekana yeye kashindwa kwenye vita hii, ila alitaka kunionesha kuwa bado ninakosa, ila kuiondoa chuki yangu kwake aliamua kuniambia kitu ambacho kinaishi mpaka Leo. Alisema kitu ambacho kwangu mimi nilikiona ni kikubwa sana. ” Kiyumbi mwanangu usione nakupiga ukadhani nakuonea sana, nataka kukumbusha kuwa kichwa chako ni muhimu sana, naomba ukitumie kichwa chako kujiongoza mwenyewe, uone hiki kitu ni kibaya hiki ni kizuri. Hiki kinaweza kunijenga na hiki kinaweza kunibomoa. Matumizi ya kichwa kwa usahihi ni kitu cha muhimu sana, na ukianza kutumia kichwa chako kwa usahihi hutosikia nimeinua mkono wangu kukupiga zaidi ya kukusalimia na kukupa pongezi kwa kutumia kichwa chako kwa usahihi. Kichwa kikikatika miguu hukanyaga popote”.
Alimalizia kwa msemo ambao ulikuwa mzito, tangu siku hiyo nilikuwa makini sana na matumizi ya kichwa changu. Niliogopa kuruhusu miguu yangu ikanyage popote kwa sababu kichwa changu kilikatika. Nilikuwa kwenye misingi hiyo, misingi ambayo imeniongoza mpaka sasa na bado naendelea kufuatilia mpira. Mpira ambao kwangu nimeufanya kama biashara, natumia mikono yangu na kuna wengine wanatumia miguu yao.
Kuna miguu mingi sana ya wachezaji wengi sana hapa Tanzania ambayo nishawahi kuishuhudia. Kati ya miguu bora ya kushoto niliyowahi kuishuhudia ni ya Ramadhani Singano “Messi” na Farid Mussa. Sema mguu wa Singano unajeraha kubwa ambalo halina mwangalizi, jeraha ambalo limeanza kuleta uozo, baada ya muda mfupi mguu utakatwa hatotembea tena huyu. Tutambakiza Farid Mussa ambaye mguu wake wa kushoto unajeraha ambalo linatibiwa vizuri kwa madaktari bora kinachobaki ni uangalifu wake ili kulitunza hilo jeraha lipone kabisa.
Kuna vijana huwa nawatazama naumia sana , kuna miguu Mungu aliiweka kwenye vichwa vibovu. Miguu ya Ajib iliwekwa kwenye kichwa kisichojitambua, kimekataa kabisa kutambua kuwa chenyewe ni nani na kinafaa kuwepo wapi kwa sasa.Miguu ya Ramadhani Singano iliwekwa kwenye kichwa kisichokuwa na washauri wazuri. Washauri ambao tangu mwanzo hawakutaka kumuonesha njia sahihi ya yeye kupita.Miguu ya Said Ndemla iliwekwa kwenye kichwa cha mtu asiyejituma, mtu anayeona alipofika ndiyo sehemu sahihi. Huyu karidhika taratibu tunasogeza siku zake za kwenda kumalizia soka lake Mtibwa Sugar asipokuwa makini!.
Hakuna hata anayepata wivu na kichwa cha Simoni Msuva, kichwa ambacho kimebebwa na kiwili wili chenyw miguu ya kawaida sana.Miguu ya Simon Msuva siyo bora kulinganisha na miguu ya Mrisho Ngassa lakini kichwa cha Simon Msuva ni bora kuzidi kichwa Cha Mrisho Ngassa. Ni miguu ambayo haichoki kwa sababu kichwa chake kimebaba akili ambayo inamfanya Simon Msuva ajitume na ajitambue. Ana maono, anaona mbali hajakubali kuridhika sehemu ambayo yupo, yeye kila siku anaipigani kesho iliyo bora, sawa hana miguu bora sana kama ilivyokuwa miguu ya Mrisho Ngassa lakini anaweza kufika mbali zaidi , sehemu ambayo Ngassa hakufanikiwa kufika. Leo hii Ngassa alitakiwa kuwa Samuel Etoo wetu kwa sasa. Lakini alikikata kichwa chake na miguu ikawa inakanyaga popote!.