- Safari ya Yanga, Mikononi mwa Dube
- Simba na Yanga nani anaongoza kuweka mpira kwapani.
- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
Tanzania imefudhu kwa mara ya kwanza toka mwaka 1979 kushiriki ama kupambana kwenye michuano ya Mataifa Afrika kwa mwaka huu ambayo itafanyika nchini Misri kuanzia Juni.
Jambo ambalo mpaka sasa kila mmoja amekuwa akiwaza ni namna gani kocha Emmanuel Amunike ataunda kikosi chake kwa ajili ya michuano hiyo ambayo itashirikisha jumla ya nchi 24 kwa mara ya kwanza toka kuanzishwa kwake.
Miongoni mwa majina ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele sana kujumlishwa kwenye kikosi hicho cha Taifa Stars ni pamoja na Ibrahim Ajib wa Yanga, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam na wengine wengi ambao wanacheza ligi ya ndani.
Lakini kwa wachezaji ambao wanasakata kabumbu nje ya Tanzania imekuwa wazi ikifahamika wale ambao wanaitwa labda kutokana na chimbuko lao la kuanza maisha ya soka hapa nchini pengine ndio maana wanatambulika zaidi hata na shirikisho la kandanda nchini ‘TFF’.
Huko nchini Austria katika klabu ya SK Sturm Graz kuna Mtanzania mwenye umri wa miaka 19 ambaye, mwenye ndoto ya kucheza timu ya Taifa ya Tanzania lakini kwa sasa akiwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana ya Austria.
Michael John Lema mzaliwa wa Itigi mkoani Singida ambaye alipata nafasi ya kwenda kusoma nchini Austria na kuishia kwenye soka, amekuwa na mtiririko mzuri licha ya umri mdogo alionao katika klabu yake hiyo.
Kutokana na kipaji ambacho amekuwa akikionesha, mwezi Februari mwaka huu klabu hiyo iliamua kumuongeza mkataba kwani tayari amekuwa lulu kwa kila mechi ambayo anashuka dimbani kucheza.
Kwa msimu huu pekee John Lema akiwa miongoni mwa Waafrika wachache kwenye klabu hiyo amecheza zaidi ya michezo 12 akifunga mabao mawili licha ya nafasi ya kiungo mshambuliaji ambayo amekuwa akicheza, mbali na hilo pia ameisaidia timu yake kuingia kwenye sita bora kwa ajili ya kupambania nafasi ya kucheza michuano ya Uropa ligi.
Mwenyewe amewahi kuripotiwa kuwa anandoto ya kucheza kwenye timu ya Taifa ya Tanzania “Nitafurahi sana iwapo siku moja nitaitwa katika Timu ya Taifa ya Tanzania, kwani Huko ndio Nyumbani kwetu, Wazazi wangu wapo huko, familia yangu na ndugu zangu wapo huko, ila shida ni kuwa tayari nimeshachukua uraia wa Austria lakini ikiwezekana kuitwa Taifa Stars nitafurahi sana” amesema.
Licha ya kuchukua uraia wa Austria naamini kutokana na umri wake na kipaji chake basi Tanzania itamuangalia kwa jicho la tatu ili kuweza kumjumuisha kwenye kikosi kitakachopambana kwenye kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Kenya.
Kwa kanuni za shirikisho la Kandanda ulimwenguni (FIFA) bado Tanzania inayonafasi ya kumtumia kinda huyu na kuiletea nchi mafanikio makubwa lakini pia kumfanya mchezaji huyu kupanda chati kutokana na kuichezea timu ya Taifa.