NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Samatta usiku wa kuamkia leo alifunga magoli mawili ya harakaharaka dakika za mwisho na kuirudisha timu yake ya KRC Genk kileleni mwa msimamo wa ligi kuu Ubelgiji baada ya kuichapa Royal Antwerp mabao 4-2.
Genk walipata ushindi huo wakiwa ugenini na sasa wapo mbele kwa alama tatu zaidi ya mabingwa watetezi Club Brugge. Genk wamefikisha pointi 33 baada ya kucheza michezo 12 na wanabaki kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo katika ligi hiyo.
MECHI 24 PASIPO KUPOTEZA
Genk tangu walipoanza msimu katika michuano ya ligi ya ulaya ( Europa League) mwezi Agosti hadi sasa November hawajapoteza mchezo wowote kati ya 28 waliyocheza hadi kufikia jana.
Wamecheza jumla ya michezo 11 katika Europa League ( Mechi nane hatua ya mtoano na nyingine tatu katika hatua ya makundi), Mechi moja ya kombe la Ubelgiji ( FA) na nyingine 12 katika ligi kuu. Kwa mwendo walionao wanaweza kushinda chochote mwishoni mwa msimu huu.
MECHI 20, MABAO 20 YA SAMATTA
Samatta alifunga magoli saba wakati wa michezo ya mtoano katika ligi ya ulaya, na tayari amekwishafunga magoli mengine matatu katika michezo mitatu ya hatua ya makundi. Kiujumla amecheza michezo kumi na kufunga magoli kumi katika michezo kumi ya ligi ya ulaya kati ya Agosti hadi Oktoba.
Pia, nahodha huyo wa Taifa Stars amecheza michezo kumi na kufunga magoli kumi katika ligi na kufanya jumla ya michezo 20 na magoli 20 katika michuano yote- takwimu bora zaidi kushinda wafungaji wote barani ulaya msimu huu.