Mashabiki wa Lunyasi Simba wamepigiwa ngoma na wameanza kuicheza kwa namna inayonishangaza. Wameanza kuaminishwa hawana timu imara licha ya usajili mzuri uliofanyika.
Wanaaminishwa wana timu dhaifu dhidi ya timu nyingine. Wakaaminishwa wana kocha dhaifu na sasa wameaminishwa Tshabalala na Kapombe wamechoka.
Vyote hivi wamejaa, wapika agenda zote hizo wamekaa pembeni na kukifurahia kile walichokipika kuwaletea walaji wao. Ni huruma. Jamani hivi vitu vinaratibiwa, haviji viji tu na haviko kwenye hadhara kwa bahati mbaya. Viko kimkakati.
Inakoendea rafiki yangu Ahmed Ally atakaukwa na mate kinywani mwake. Kila uchwao anasikika katika vyombo vya habari kuitetea Simba SC, ni kama vile Simba SC wana timu dhaifu inayohitaji utetezi.
Hapa wapika agenda wamefanikiwa. Kinachofanyika sasa Simba SC, mashabiki hawaoni kinachofanyika katika timu yao. Sijui kama hata wanajua wana alama 9 sawa na vinara (tofauti ni magoli).
Nawasikitia mashabiki hawa ambao wana timu imara ya ushindani, lakini wameingizwa kingi na wameingia, tena kiurahisi tu.
Simba Sc wana timu ikara na bora msimu huu kuliko misimu mitatu nyuma.Wameshinda kikombe cha Ngao ya Hisani pale Tanga, tena kwa kumfunga Yanga SC. Hili ni taji ambalo hawajaichukua kwa misimu miwili.
Simba SC watashiriki mashindano ya Super Cup (Afrika Mashariki wanashiriki wao tu). Mpaka sasa wana Jean Baleke aliyefunga mabao 5 katika ligi. Ni yeye anayeongoza.
Vyote hivi hawavioni, wanakuja mbele ya hadhara kulaumu mambo yanavyokwenda klabuni. Hii sio sawa. Ni kuwakosea heshima viongozi wenu waliofanya usajili huu.
Kwanini simba wanakata tamaa mapema, sidhani kama ni muda muafaka wa kukata tamaa hii.