Nilipopata taarifa hii ya kukwama kwa klabu ya Majimaji jijini Dar ,akili yangu iliganda nikarejea miaka 15 na ushee iliyopita nyuma nilipopata kuichezea timu hii kwenye ngazi ya ligi kuu
Hapa unielewe naimba wimbo ninao ufahamu ,nikiwa mchezaji wa timu hii nilipata kupitia kadhia hizi za kukwama ugenini kwa madai ya uongozi haujapata fedha kwa ajili ya kuendesha timu kutoka kwenye vyanzo vyake
Kwa kiasi fulani kikubwa tu football ya nchini mwetu imestaarabika na kupiga hatua kadhaa mbele
Ligi kuu ndiyo haswaaa imesonga hatua 20% mbele toka zile 40 % tulizokuwa nazo na kwa sasa tunazo 60%
Majimaji ya Songea timu iliyowahi kupeperusha Bendera ya nchi kimataifa.
Binafsi nimebahatika kucheza timu kadhaa kwenye ngazi ya ligi kuu lakini kiuhalisia hii ndiyo timu ninayoipenda zaidi kutokana na kuniamini na kunipa nafasi nikiwa kinda ( mvulana wa wakati huo) na hata game yangu ya kwanza (first debut) katika ngazi hiyo niliifanya nikiwa na timu hiyo dhidi ya Simba
Leo ni miaka mingi sana imepita lakini matatizo ya timu ni yale yale
Na inawezekana matatizo hayo ndiyo yanafanya timu ishuke kutoka daraja moja kwenda jingine hadi sasa kuwa daraja la pili pamoja na kuitwa’ first division league’
Katika muda ambao Majimaji haitendewi haki ni muda huu,mara nyingi vilabu huwa vinatelekezwa ni wakati havifanyi vizuri kwa maana ya kupata matokeo
Majimaji licha ya kukosa nafasi ya kwenda kucheza hatua ya 8 bora mjini Mwanza
Bado imepambania sana hadhi ya mkoa wa Ruvuma katika michezo yao ya mwishoni ikiwemo kushinda michezo miwili ya mwisho ugenini dhidi ya Baga Freshi ya Pwani bao 3-0 na ule wa uliowaleta Dar vs Dar City walioshinda 3-2
Leo uongozi unatajwa kuwatelekeza wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi waliokuja na timu
Ikielezwa tatizo la kwanza linaanzia kwenye makubaliano ya basi lililo waleta hapa Dar ilipaswa kuja na kugeuza nao lakini hakulipwa chochote zaidi ya kishika ‘ uchumba kidogo’ wasomi wanasema Advance
Sakata la pili ni kufukuzwa Guest house waliyofikia na kwenda kuishi kwa Msamariamwema
Hofu yangu kubwa ni kwa wachezaji wenye umri mdogo huwenda wakaukatia tamaa mchezo huo wakudhani kote maisha yatakuwa hivi hivi
Majimaji mnaenda wapi? Sidhani kama huwa wanakaa vikao vyenye tija kutathimini mwenendo wa timu kwenye kuporomoka toka ngazi moja kwenda nyingine
Pamoja na yote uongozi na wadau wa timu ya Majimaji ‘Wanalizombe’ Wafanyabiashara Wanasiasa kutoka mkoa huo mnapaswa kuinusuru timu hiyo kurejea nyumbani
Kwa sisi wakazi wa Dar tunauzoefu mkubwa sana pale tunapofikwa na mgeni mwanafamilia moja au wawili kwa wakati moja toka mikoani zilipofamilia zetu
Sembuse Msamariamwema anayekaa na timu ambao si nduguzake wa karibu?
Si vibaya nikiweka mawasiliano ya Meneja wa timu kama utakuwa na mchango Fedha mawazo nk 0674703248
Ila binafsi yangu imenisononesha sana kwa kuwa nilifanyiwa haya miaka mingi iliyopita nikajua kwa Dunia ya sasa hayawezi kujirudia.
Kweli Wahenga hawakukosea kusema ‘zimwi likujualo halikuli likakwisha’