Sambaza....

Aliwahi kujisemea mwendawazimu mmoja kuwa shetani akizeeka anageuka Malaika. Rafiki zangu wa Liverpool zamani walikuwa wakiishi kishetani, lakini sasa wanaishi Kimalaika. Muda sio rafiki mzuri tena kwao.

Zamani enzi za zama za mawe Liverpool walikuwa na kocha wao aliyekuwa akiitwa Bill Shanky. Shanky hakuwa kocha tu, alikuwa kama baba katika timu, alikuwa kama mfalme katika timu, alikuwa kiongozi anayeamlisha watu na watu kumtii. Shanky alikuwa kila kitu Liverpool.

Katika jukwaa moja la Uwanja wa Anfield wanalokaa wahafidhina wa Liverpool ‘The Kops ‘ mpaka leo wanamuona Shanky ni kama alikuwa Mungu wao na hakuwa kocha kama ulivyosema mkataba wake. The Kops huwa wanalipamba jukwaa lao kwa picha zake na hawachoki kulitaja jina lake.

Image result for Bill Shankly

Shanky aliijenga Liverpool kuwa ya timu ya kiume na ikawa kweli. Aliwafanya wachezaji wote wa Liverpool, wajisikie fahari kuivaa jezi yao na kuitumikia. Kando ya mataji wanayosotea Liverpool siku hizi, vitu pekee walivyoachiwa na Shanky ni ule upambanaji wao na kile kibao cha This is Anfield. Wamebaki na vitu hivyo viwili muhimu, lakini hawana tena timu.

Moja ya matukio makubwa ya Shanky yaliyowahi kutikisa nyufa na kuta za Anfield ni kumtamkia mmoja ya wachezaji wa Liverpool kuwa mguu wa mchezaji ni mali ya Liverpool.

Mchezaji huyo alivunjika mguu na asingeweza kuendelea na mchezo, hivyo aliomba kutolewa ili nafasi yake ichukuliwe na mchezaji mwingine, Shanky alimfuata mchezaji huyo na kumkolomea na kumwambia maneno hayo.

Leo Liverpool wagumu uwanjani na bado wana damu ya Shanky, lakini hawana tena timu ya wanaume majasiri. Hawana wachezaji ambao mchezaji wa mpinzani akiweka mguu wao wakaweka vichwa. Hawana tena wanaadamu wa aina hiyo. Tunavyowaona hawajachukua ubingwa kwa miaka 25, sio kwa bahati mbaya. Kuna kitu hakipo, kinapaswa kurudishwa.

Philipe Countinho ni fundi wa mpira na dunia inalijua hili, lakini ni kama anawaangusha Liverpool baadhi ya maeneo, leo hii analilia kuondoka, angewezaje kuipuuza Liverpool enzi za Shanky kama anavyoipuuza sasa?

Anyway dirisha dogo limefunguliwa na Liverpool wamevunja ukimya. Wameamua kuikumbusha dunia kuwa wao ni Liverpool wenye nembo ya jogoo kwenye jezi zao.

Virjik Van Dijk

Wametoa kiasi kikubwa cha pesa kumnunua mlinzi wa kati wa Southampton, Virjik Van Dijk. Wamelipa Paundi Milioni 75. Unapotaka kuwa bingwa wa Uingereza na Ulaya (UEFA ) unapaswa kufanya sajili za kichaa namna hii bila kujali pesa.

Hapa naweza kupokea lundo la maswali juu ya Leicester City na ubingwa wao wa maajabu. Leicester walitembea na Mungu wa bahati katika msimu ule ambao Chelsea, Arsenal, Manchester United, Manchester City zote zilikuwa hovyo.

Image result for LIVErpool fc wins premier league

Heshima ya Manchester City na Chelsea, ilikuja kwa pesa, haikuja kwa mikwara na mikemeo kama ya Shanky kwenye enzi zile za zama za mawe. Pesa ni sabuni ya roho.

Kila timu inajitafutia njia ya ubingwa kwa inavyojua. Wakati Liverpool wakitoa pesa nene kwa beki, Arsenal wameamua kuwa na mkono wa birika kwa kumsajili beki kwa Paundi Milioni 2. Duniani hakuna kaburi la mjinga.

Unadhani Arsenal wako pale walipogotea kwa bahati mbaya? Bao hawako kwa bahati mbaya. Inavyoonekana akili ya kocha wao Arsene Wenger imeshachoka na anachoweza kukifanya kwa ufanisi ni kufunga na kufungua zipu ya lile koti lake refu jeusi.

Jürgen Klopp, kocha wa Liverpool

Katika zama zile za Shanky mpaka hivi sasa, kuna mchezaji wa Paundi Milioni 2 anayeweza kukupambania kukupa ubingwa mwishoni mwa msimu?

Mpaka ikifika siku ya mwisho ya dirisha hili dogo kufungwa, kila shabiki atakuwa ameshafahamu timu yake itamaliza msimu katika nafasi ya ngapi, kabla ya kufikia huko Mei. Mzaramo aliwahi kujisemea Zuwa Diswa!

Sambaza....