Timu ya soka ya Liverpool inatakiwa kujiandaa kiume pale itakapowafuata wanaume wa kazi Bayern Munich kwenye uwanja wa Allianz Arena katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya 16 bora mkondo wa pili baada ya kutoka sare ya 0-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza.
Beki wa kati wa majogoo hao wa Anfield Van Dijk amesema ni lazima wapambane kiume na ugumu huo wanaufahamu hasa ukizingatia Bayern Munich sio ya mchezo mchezo wanapokuwa nyumbani kwao.
Dijk amesema hawakuwa kabisa na matokeo mazuri ya ugenini kwenye hatua ya makundi na hilo ndilo ambalo linazidi kuufanya mchezo huo utakaopigwa kesho kuwa mgumu kwao ukijumlisha na matokeo waliyoyapata katika mkondo wa kwanza.
“Michezo ya hatua ya makundi haikuwa vizuri kama vile tulivyohitaji, lakini muhimu tumefika kwenye hatua ya mtoano, najua utakuwa ni mchezo mgumu na sisi tunakuwa kuwa bora kuliko tulipokuwa kwenye michezo ya ugenini kwenye hatua ya makundi,” Dijk ameviambia vyombo vya habari vya Uingereza.
Liverpool ilipoteza michezo yote ya ugenini kwenye hatua ya makundi (Napoli 1-0, Red Star Belgrade -2-0, PSG 2-1) jambo ambalo limeendelea kumtesa beki Vijk akifikiria mchezo huo wa hapo Jumatano “Tunataka kufanya kila kitu kilicho kwenye uwezo wetu ili tuvuke hatua hiyo, kutakuwa na kipindi ambacho tutakuwa na pressure kutokana na ubora wa wachezaji wao, lakini pia na sisi tutakuwa na muda wetu kwani na sisi tunawachezaji bora” amesema.
Liverpool ambayo ilicheza fainali msimu uliopita na kupoteza mbele ya Real Madrid, itahitaji ushindi wa aina yoyote ama sare ya mabao ili kuweza kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo barani Ulaya.