Baada ya tetesi kuenea kuwa Mechi kati ya Simba na Lipuli iliyobadilishwa ratiba, imeombwa kuchezwa kama ilivyopangwa awali, Msemaji wa Lipuli Fc, Clement Sanga, amekanusha.
Ratiba ya mechi hii ilibadilishwa kutokana na kambi ya timu ya Taifa, ambayo ilikuwa na wachezaji wengi wa klabu ya Simba Sc, ambao kwa sasa wameondolewa baada ya kuchelewa kuripoti kambini.
Taarifa ya Lipuli Fc hii hapa:
Kwa niaba ya uongozi wa klabu ya Lipuli Fc napenda kuchukua fursa hii kukanusha vikali taarifa inayozunguka kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii inayosema viongozi wa klabu ya Lipuli Fc na klabu ya Simba SC kwa pamoja wameliandikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba mchezo unaovihusu vilabu hivyo uchezwe kama ulivyopangwa hapo awali. Taarifa hiyo ni uzushi na ina malengo ya kuzua taharuki miongoni mwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu yetu. Ningeomba taarifa hiyo ipuuzwe mara moja. klabu ya Lipuli Fc haijakaa na klabu ya Simba SC kuliandikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Ikumbukwe mchezo baina ya klabu ya Lipuli Fc na Simba SC ulipangwa kuchezwa tarehe 2 Septemba jijini Dar Es Salaam lakini umesogezwa mbele na utapangiwa tarehe nyingine.
Imetolewa na Afisa Habari wa klabu ya Lipuli Fc, Clement Sanga.
Simba Sc kwa sasa anaongoza Ligi Kuu na imetoa mchezaji mwenye magoli mengi hadi sasa, Meddie Kagere.