Sambaza....

Mshambuliaji kinda wa Singida United Habibu Haji Kyombo huenda akajiunga na Mamelodi Sundowns baada ya kufanikiwa majaribio ya siku 20 aliyoyafanya na klabu hiyo ya nchini Afrika Kusini.

Meneja wa klabu ya Singida United Festo Richard Sanga amesema mchezaji huyo ambaye awali alikwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya majaribio ya siku 10, aliweza kuwavutia benchi la ufundi la Mamelodi na kumuongezea siku nyingine 10 ili kuweza kumuangalia vizuri.

Sanga amesema katika siku 10 za Mwanzo Kyombo aliweza kufanya majaribio kwa ufanisi mkubwa na timu ya vijana kabla ya kuhamia kwenye timu ya wakubwa ambapo napo aliweza kufanya vizuri hadi ikapelekea viongozi wa Mamelodi kuomba kuzungumza nao ili kuweka mambo sawa.

“Takribani siku 20 Habibu amekuwapo kwenye kikosi cha Mamelodi, alianza kufanya majaribio na timu na timu ya vijana lakini baadae akaungana na timu kubwa na watu wa Mamelodi kimsingi kwa ripoti ambazo sisi tumeshaipata ni kwamba wamependezewa na huduma ya mchezaji, umri alionao na kiwango alichonacho,” Sanga amesema.

“Na kimsingi wameahidi kuwa watahitaji kufanya mazungumzo ya kina kati yetu sisi na wao, kwa hiyo tunawasubiria Mamelodi Sundowns ili pale watakapokuwa tayari basi sisi hatutakuwa na kinyongo, na kiukweli tumefurahi kwa wakati wote ambao Kyombo alikuwa Afrika Kusini hakuwa na matatizo yoyote,” Sanga amesema.

Mbali na hilo Sanga amesema pia hivi karibu watawapeleka wachezaji wengine wawili nje ya nchini ambapo mmoja kati yao atakwenda Jamhuri ya Cheki na amesema itakuwa mapema sana kwa sasa kumtangaza.

Sambaza....