Sambaza....

Wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia katika michuano ya Caf, Simba SC jioni ya Leo watatupa karata yao ya mwisho ili kujaribu kupindua matokeo ya 1-2 vs Nkana Red Devils FC na kufuzu kwa hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika 2018/19

‘ Wekundu wa Msimbazi’ walipoteza walikuwa nyuma kwa mabao 2-0 kwa zaidi ya dakika 75 kabla ya mshambulizi Mnyarwanda, Meddie Kagere kutumia uzoefu wake kumdanganya mwamuzi na kuipatia penalty timu yake ambayo ilikwamishwa nyavuni na nahodha John Bocco dakika kumi kabla ya kumalizika kwa mchezo.

PASI ZA NYUMA

Jonas Mkude kama ilivyo kawaida yake alipiga pasi kadhaa zisizo na mwelekeo katika mchezo wa kwanza mjini Kitwe Jumamosi ya wiki iliyopita, haitoshi kiungo huyo mwenye jukumu la kupandisha timu na kusaidia ukabaji alicheza pasi nyingi za kurudi nyuma.

Akitaraji kuwapanga, Mkude, Mghana, James Kotei na Mzambia, Chollo Chama katika eneo la kiungo kocha Mbelgiji, Patrick Aussems atalazimika kusimama mara kwa mara katika eneo lake ili kumpigia kelele Mkude.

Chama licha ya kwamba ndiye kiungo aliyekuwa na ubora zaidi katika kikosi cha Aussems kabla ya mchezo wa kwanza alizimwa na wala hakuwa tishio kwa ‘Mashetani Wekundu’ hao wa Zambia. Alulazimika muda mwingi wa mchezo wa kwanza kusaidia ulinzi badala ya kuchezesha timu.

Nkana walipokuwa wakiwasili.

Stahili ya uchezaji ya Mkude (kupendelea kukaa sana na mpira), pasi zake mkaa za kurudi nyuma ni kati ya mambo yanayoweza kuwapa faida Nkana katika mchezo wa Leo. Anatakiwa kucheza kama Kotei, kupiga pasi sahihi kwa wakati, na kutopoteza mpira mara kwa mara.

Kwa timu yenye wachezaji wanaocheza kwa kasi kama Nkana kucheza ‘ back pass’ mara kwa mara kwa mchezaji wa nafasi ya kiungo ni hatari sana kwa Simba.

ULINZI

Nkana walifunga magoli mawili mjini Kitwe dhidi ya beki ya Mghana, Nikolas Gyan, Muivory Coast, Paschal Wawa, Erasto Nyoni na Mohamed Hussein’Zimbwe JR’ wiki iliyopita, lakini nao waliruhusu goli katika lango lao.

Kwa aina ya uchezaji na washambuliaji walio nao, Nkana wataendelea kuwa tishio kwa safu ya ulinzi ya Simba katika mchezo wa Leo ndani ya uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nadhani kuna ulazima wa kocha Aussems kufanya mabadiliko katika ngome yake.

Nkana Fc

Kwanza anapaswa kumuondoa kikosini Gyan na nafasi yake kuchukuliwa na Nyoni ambaye katika mchezo wa kwanza alicheza katika beki ya kati sambamba na Wawa, pili, Aussems analazimika kumrejesha kikosini Mganda, Jjuuko Murshid ili acheze na Wawa katika eneo la kati.

NI MAKOSA KUWAPANGA PAMOJA, OKWI, BOCCO, KAGERE

Mwanzoni kabisa mwa msimu Aussems alijaribu kuwapanga kwa wakati mmoja mastraika wake wote watatu-Mganda, Emmanuel Okwi, nahodha Bocco na Kagere, lakini kwa sababu za kitimu kuwanga kwa pamoja washambuliaji hao ni makosa.

Ni makosa zaidi hasa pale unapokutana na wapinzani wanaojiamini na kushambulia kama Nkana FC. Hasara ya kuwapanga kwa wakati mmoja mastaa hao watatu ni kwamba, timu itabaki pungufu wachezaji wawili wakati inaposhambuliwa.

Okwi, Kagere, Bocco wote si wakabaji na wachezesha timu wazuri kuliko, Shiza Kichuya. Nadhani, Aussesms anapaswa kumpa nafasi ya kuanza mchezo mmojawapo kati ya raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima, Kichuya ama Hassan Dilunga na kumuacha nje mmoja kati ya Okwi, Meddie au Bocco ili timu yake ibalansi kiulinzi na mashambulizi.

GOLI LA UGENINI

Inafahamika kuwa goli la ugenini hutumika pale matokeo yanapokuwa pacha baada ya dakika 180 kumalizika.

Simba tayari wapo nyuma 1-2, ushindi wa 1-0 unaweza kuwapeleka hatua ya makundimabingwa hao wa Tanzania bara lakini katika uchezaji wa timu zote hata Nkana wanaweza kufunga na kupita kwa goli la ugenini jijini Dar .

Timu hiyo ya Zambia inaweza kufunga kutokana na kuwa na wachezaji wazuri katika mashambulizu. Beki na nyanda wa Simba wanaweza kuwaondoa mashindanoni kama itaendelea kupangwa vibaya na kukabia macho.

NANI MSHINDI?

Nawaona wageni wakifuzu kwa hatua ya majundi Leo. Sare ya kugungana au ushindi wa 3-2 wa Simba utawavusha Nkana hadi hatua ya 16 bora.

Sambaza....