“Kiyumbi , hutakiwi kufikiria ni kitu gani utaachia watu baada ya wewe kufa, unatakiwa kufikiria ni jinsi gani utakavyoendelea kuishi ndani ya watu baada ya wewe kufa”.
Hiki ndicho kitu ambacho huwa sikisahau kutoka kwenye kinywa cha ndugu yangu Israel Saria, mtangazaji nguli wa BBC Swahili.
Mtu ambaye anapenda sana kufikiria namna ambavyo kila kazi inavyoweza kuishi ndani ya watu. Inavyoweza kuishi milele.
Namna ambavyo maisha ya mwanadamu yanaweza yakaacha alama kubwa ambayo inaweza kudumu kizazi hadi kizazi.
Tunawakumbuka kina Pele kwa sababu tu miguu yao waliitumikisha ipasavyo , miguu yao ilisababisha tuwaweke kwenye mioyo yetu.
Miguu yao iliwafanya leo hii tuwakumbuke na kuwaandika kama Wafalme wa soka duniani. Hizi ni alama.
Alama ambazo zinaishi mioyoni mwa watu. Waliwekeza kwa watu , hawakufikiria kuwekeza kwenye vitu ambavyo havitodumu.
Kuna siri moja ambayo wengi huwa tunaisahau. Watu wengi mashuhuri au viongozi mashuhuri ambao hukumbukwa kila uchwao, hawakuwahi kuanza kufikiria kuwekeza kwenye vitu.
Wao walianza kufikiria namna ya kuwekeza kwa watu. Hiki ndicho kitu cha kwanza ambacho walianza kufikiria kabla ya vitu vyote.
Yesu alifikiria kuanza kuwekeza kwa watu kwanza kabla ya kuanza kuwekeza kwenye majengo. Na ndiyo maana mpaka sasa hivi tunamkumbuka sana Yesu.
Kwanini ?, aliwekeza kwa watu. Aliwekeza kwenye hisia za watu. Aliacha alama kwenye mioyo ya watu wengi.
Hii ndiyo siri kubwa ya kwa mwanadamu yeyote yule kuweza kukumbukwa kila uchwao. Kwa mwanadamu yeyote kukumbukwa na vizazi vyote duniani.
Mhuri unaopigwa kwenye mioyo ya wanadamu siku zote huwa siyo rahisi kufutika. Ni ngumu kwa mihuri hii kufutika.
Mwanadamu anaweza kujichora ” tatoo” kwenye mkono wake, mgongoni, tumboni , shingoni lakini akaja kuifuta au kuibadilisha baada ya siku kadhaa.
“Tatoo” ya moyoni haibadiliki wala kufutika kirahisi hata siku moja. Ukipiga “tatoo” kwenye mioyo ya watu itasimama milele.
Na hizi “tatoo” za kwenye mioyo ni mara chache sana kutokea. Na wengi huwa hatuziweki ingawa watu wengi huwa wanatamani kupigwa “tatoo” ya moyo.
Unajua kwanini ?, “tatoo” ya moyo hupigwa bila maumivu. Anayepigwa hupigwa huku akiwa anatoa tabasamu.
Hakunji uso kwa maumivu, hutoa tabasamu pana huku chozi la furaha likiteremka. Tukio kama hili ni ngumu kufutika kabisa kwenye akili ya watu.
Na huu ndiyo mtihani mkubwa ambao timu yetu ya Taifa Stars iliyobaki nao muda huu. Mtihani wa wao kutupiga tatoo kwenye mioyo yetu.
Mioyo yetu iko tayari kwenye hili.