Kocha mkuu wa wekundu wa msimbazi Patrick Aussems ameshindwa kuweka wazi kuhusu taarifa ya ugomvi wake na kocha msaidizi Masoud Djuma hadi kufikia kushinikiza kuomba kocha huyo aondolewe kwenye kikosi chake.
Aussems amesema hana taarifa zozote za ugomvi huo kwani kama zimekuwa zikiandikwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti nchini basi hajawahi kuzisoma kwani mbali na kutojua Kiswahili lakini yeye sio mpenzi sana wa mitandao ya kijamii.
“Unajua mimi siwezi kusoma Kiswahili, hivyo siwezi kusoma magazeti ya hapa, kwa hiyo sina lolote la kuongelea kuhusu hilo, kitu muhimu kwetu kwa sasa ni kuzungumzia mechi zilizombele yetu, na wachezaji ndio watu muhimu kwetu kwa sasa,” Aussems amesema.
Kocha huyo ambaye ameshaiongoza Simba katika michezo miwili ya ligi akifanikiwa kushinda yote amedaiwa kuwa na maelewano hafifu na kocha Masoud na imetajwa kuwa kocha huyo tayari ameoneshwa mlango wa kutokea kwa wekundu hao wa Msimbazi.
Taarifa zilisema kuwa Aussems alimtaja Masoud kama muanzisha mgomo kwa wachezaji wa timu hiyo ili wacheze chini ya kiwango ili yeye afukuzwe na Masoud kuchukua nafasi ya kuwa Kocha mkuu wa Kikosi hicho ambao ni washindi wa Ngao ya Jamii.
Katika Hatua nyingine Aussems amesema kikosi chake kinaendelea vizuri na maandalizi ya michezo ijayo ya ligi lakini ameilalamikia ratiba ya ligi kwani wakiwa mwanzoni kabisa mwa ligi wanapumzika kwa takribani wiki mbili kabla ya kuendelea tena.
“Tunahitaji kuheshimu hizi taratibu, lakini tutakaa kwa kama wiki mbili hivi bila kucheza mchezo wa kimashindano, nafikiri hili ni jambo la ajabu sana hasa ukiangalia ni mwanzo mwa ligi,” amesema.
Simba inaendelea na mazoezi na wachezaji wake wote isipokuwa kwa wachezaji Cletus Chama, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima na Jjuuko Murushid ambao wapo katika majukumu ya timu zao za Taifa.