Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Amri Kiemba Ramadhani ametoa maoni katika kipindi cha redio cha “hili game” kuhusu kikosi cha timu ya Taifa kilichoitwa jana.
Kiemba mchezaji wa zamani wa Simba na Stand United amesema timu ya Taifa ni mradi wa muda mrefu na sio kwaajili ya mashindano pekee.
Amri Kiemba “Timu ya Taifa ni “project” sio mashindano Mwalimu ili kujilidhisha ni lazima amuite ili amuone uwanjani kama huyu anatufaa au hapana na kwa sababu ni mradi Mwalimu ndio anaona hata kama hamtumii atamwambia nini afanye kurudi kwenye mstari”
Kiungo huyo pia aliongeza hata yeye aliwahi kuitwa timu ya Taifa wakati alikua hapati nafasi katika klabu yake ya Simba hivyo si ajabu kwa Feisal kujumuishwa timu ya Taifa.
“Mwisho wa siku ni Mchezaji wa timu ya Taifa huwezi kumuacha kwa sababu hachezi , hata mimi nimecheza timu ya Taifa wakati nilikuwa sichezi timu ya Klabu, kipindi nipo Simba kuna wakati timu ilikuwa inashikiliwa na Makocha na nilikuwa sipati nafasi, nikiitwa timu ya Taifa naanza na nakuwa miongoni mwa waliofanya vizuri,” alisema Amri Kiemba.
Mwalimu Adel Amrouche ameita kikosi cha wachezaji 31 ambao wataingia kambini kujiandaa na michezo miwili ya kufuzu Afcon dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda “The Cranes”.