Tarehe 4/1/2020 inakaribia sana. Siku ambayo nchi nzima itasimama kushuhudia pambano moja ambalo hugawa nchi pande mbili. Upande wa kwanza ni Yanga upande wa pili ni Simba.
Hawa ndiyo wakubwa wa mpira hapa nchini na mechi yao hugusa hisia za watu wengi sana. Mechi hii inaonesha ni ya upande mmoja kwa sababu Simba wanaonekana wako vizuri sana kuzidi Yanga kuanzia nje ya uwanja na ndani ya uwanja. Kuna vitu ambavyo kimsingi Yanga wanatakiwa kuwa navyo ili kuwapa nafasi ya kushinda hii mechi.
YUSUPH MANJI
Huyu aliwahi kuwa mwenyekiti-mfadhali wa klabu hii , kipindi chake Yanga ilikuwa tishio sana. Tangu aondoke Yanga imekuwa na unyonge sana. Haifanyi vizuri ukilinganisha na kipindi chake kwa sababu kipindi chake kila huduma ilikuwa inapatikana kwa wakati, mshahara , kambi bora na motisha kwa wachezaji.
Kwa sasa Yanga hawana mtu wa kuyafanya vyote hivi. Mpira bila pesa hakuna mafanikio , na mechi hii ili kushinda inahitaji hamasa kubwa sana kwa wachezaji. Yanga wanahitaji mtu mfano wa Yusuph Manji ambaye atahakikisha timu inakuwa kwenye mazingira bora.
MWINYI ZAHERA
Kocha wa zamani wa Yanga , kuna vitu viwili ambavyo kwa sasa Yanga wanavihitaji kutoka kwa kocha aina ya Mwinyi Zahera. Mwinyi Zahera alikuwa na uwezo wa kuunganisha timu na mashabiki jukwaani.
Hata kama Yanga ikiwa kwenye wakati mgumu kiuchumi lakini alikuwa na uwezo wa kuwafanya wachezaji wapigane kwenye nyakati ngumu na huku mashabiki wakiwa na nguvu na imani kubwa ya kuiunga timu.
Yanga inahitaji moyo wa kujitolea kutoka kwa wachezaji na mashabiki na kocha ni kiungo muhimu sana wa kuunganisha mashabiki na timu , Mwinyi Zahera alikuwa na uwezo kwenye hilo na kwa muda huu wanamwihitaji kocha aina ya Mwinyi Zahera kuweza kufanya hiki.
Pili Mwinyi Zahera alikuwa na uwezo mkubwa wa kuifanya timu ijilinde vizuri , mechi hii inahitaji timu yako iwe imara eneo la kujilinda na kocha wa aina hii anahitajika kwa sasa ndani ya kikosi cha Yanga.
PATRICK AUSSEMS
Kocha wa zamani wa Simba , kocha ambaye alikuwa na sifa ya timu yake kushambulia na kufunga magoli. Kama kocha wa Yanga akiwa na uwezo wa kujilinda kama Mwinyi Zahera na akafanikiwa kushambulia kama Patrick Aussems basi Yanga itakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Kwa hiyo uwepo wa nguvu hizi tatu kwa pamoja nguvu ya pesa ambayo Yusuph Manji kasimama kama mwakilishi , nguvu ya hamasa na kujilinda iliyobebwa na Mwinyi Zahera na nguvu ya Kufunga na kushambulia iliyobebwa na Patrick Aussems. Hizi nguvu tatu zikijumuishwa kwa pamoja zinaweza kuleta matokeo chanya kwa Yanga.