Kuelekea mchezo wa marudiano kati ya wenyeji Marumo Gallants dhidi ya wageni Yanga katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kocha wa Marumo Raymond Mdaka amesema hawana wasiwasi juu yakupata ushindi.
Mdaka anaona kuwa kuwafunga Yanga si jambo geni kwao. Marumo waliweza kuibuka na ushindi walipokuwa katika hali kama hiyo walipomenyana na USM Alger katika hatua ya makundi.
“Tulikuwa katika hali hii hapo awali. Kumbuka tulicheza USM Alger. USM ilionekana kuwa bora zaidi kuliko wao [Yanga], lakini siwadharau,” alisema Mdaka na kuongeza. “Lakini tunahisi bado tunaweza kuwafunga. Kwetu sisi ni kwenda katika mchezo na kupata bao la mapema. Na ni wazi, itawasumbua na kuwaweka katika presha. Na tunapambana kupata bao la pili, mradi tu tusiruhusu bao.”
Kocha huyo pia amesema mchezo wa awali waliopoteza Jijini Dar es salaam haukua mgumu sana. Yanga walipata mabao mawili kupitia kwa Benard Morrison na Aziz Ki na kupelekea kupata ushindi wa mabao mawili kwa bila katika mchezo wa awali.
“Ukiangalia pambano la mkondo wa kwanza, ni mchezo ambao tuliona kama haukuwa mchezo mgumu. Hatukuweza kubadilisha nafasi zetu na kuwa mabao.”
Kocha huyo alibainisha zaidi kuwa walikuwa na wachezaji wachache muhimu ambao walikosa mchezo wa mkondo wa kwanza. Hii ilitokana na majeraha na anaamini kikosi chake kitaongezewa nguvu na wachezaji hao katika mechi ya marudiano.
“Kuna wachezaji wachache ambao hawakuwepo. Kumbuka Ngema, Nku, na Mabotja hawakuwepo kwa sababu ya majeraha,” alimalizia Raymond
Yanga wanashuka dimbani katika uwanja wa Royal Bafokeng saa moja jioni kwa saa za Tanzania katika mchezo ambao wanahitaji sare ama kutokupoteza kwa mabao zaidi ya mawili ili kuweza kusonga fainali.