Mwanzo wake ulionesha kuwa yeye ni mtu ambaye ameumbiwa kwa ajili ya kucheza Ulaya. Alikuwa na ndoto hiyo, na alikuwa akiimba kila uchwao.
Alifanya mazoezi kwa juhudi sana, akiamini kuna siku atacheza katika ligi kubwa barani Ulaya. Alitembea na imani hiyo, nguvu za imani yake akaziweka katika miguu yake.
Macho yake hayakutaka kutazama chochote zaidi ya njia ya yeye kutoka hapa nchini. Hakutaka kabisa kucheza hapa, na alicheza hapa kwa sababu tu alizaliwa hapa na ilimbidi aanzie hapa ili aende anapopatamani.
Hakutaka kabisa kushawishika na shilingi zetu, na hakuona fahari kuvaa jezi ya moja ya mafahari wakubwa nchini katika soka. Kwake yeye jezi ya Simba ilikuwa haimanishi kuwa huo ndiyo mwisho wa safari yake.
Kila alipokuwa anavaa jezi ya Simba, ilimkumbusha kuwa yuko katika hatua yake ya kwanza kati ya hatua mia za kufikia mafanikio yake anayoyaota.
Ndiyo maana hata aliponyimwa gari, hakuona hatari kuwagomea huku akiendelea kujifua kwa nguvu. Hakusahau kuwa mpira ni kazi yake, hakuruhusu mtu yeyote kuleta utani kwenye kazi yake.
Alikuwa anaiheshimu sana!, na alikuwa ameiweka kama kitu ambacho kitakuwa na msaada mkubwa kwake kwa mbeleni. Kitu ambacho kitamfanya awe Bilionea mkubwa.
Kitu ambacho kitamfanya aheshimike sana, kwa hiyo alianza kujitambua sehemu ambayo wengi wa wachezaji wetu ni ngumu kujitambua. Ni ngumu sana kwa mchezaji wa Tanzania kujitambua akiwa Simba au Yanga!.
Wengi wao huwa wanaona kuvaa jezi ya njano au nyekundu ndiyo mwisho wa safari yao kabisa, hawana njaa ya mafanikio , hujikuta wameridhika sana. Ni ngumu kwao wao kuruhusu mguu wao kupiga hatua ya pili.
Hii ilikuwa tofauti kabisa na kwa Mbwana Samatta, hakuamini kabisa hii ndiyo sehemu yake ambayo anaweza kuiita kama kilele cha mafanikio.
Masikio yake yalikuwa yameshapata kusimuliwa hadithi ya Shaban Nonda. Aliambiwa kuwa aliwahi kukanyaga ardhi ya Kariakoo, na ikawa mwanzo wake wa kuwa mchezaji wa kulipwa.
Akili yake , nguvu zake na kila kitu chake alikuwa anafikiria namna ya kuwa mchezaji mkubwa wa kulipwa. Ndiyo maana kila alipokuwa anakanyaga nyasi za uwanja wowote alikuwa anafanya kitu akiwa na njaa sana.
Njaa yake ilianza kuonekana dhahiri kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe, alionesha kiwango kikubwa cha njaa na TP Mazembe wakamuona na kumpa nafasi.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wake mpya, ukurasa wa pili wa Mbwana Samatta ukaanzia hapo, ukawa ukurasa ambao uliwakutanisha na Mtanzania mwenzake Thomas Ulimwengu.
Ni furaha sana kwa ndugu kukutana katika nchi ya ng’ambo. Najua walikuwa wanapata muda mrefu sana wa kuongea kuhusu matarajio yao ya kucheza sehemu ambayo ni kubwa zaidi ya TP Mazembe.
Kila uchwao walikumbushana kuwa TP Mazembe siyo kituo chao cha mwisho cha safari yao. Walikuwa bado na safari ndefu kufikia kwenye mafanikio makubwa.
Kila mmoja ikambidi kupigana kwa nafasi yake ili tu wapige hatua nyingine kwenda mbele!. Alikuwa Mbwana Samatta ambaye alifanikiwa kuanza kuondoka pale TP Mazembe!.
Likawa jambo jema, ila ikabaki kuwa deni kubwa kwa Thomas Ulimwengu. Na yeye alitakiwa kuondoka!, na nafsi yake ilikuwa inauma kubaki pale wakati mwenzake yupo Ulaya.
Akili yake ikawa inawaza Ulaya, akili yake ikawa inafikiria jinsi ya kumfuata Mbwana Samatta, kitu ambacho ni sahihi. Ilikuwa wivu wenye maendeleo.
Nahisi kitu alichokosea alianza kukimbia sana bila uelekeo. Alipoona Mbwana Samatta kafanikiwa kukimbia na yeye akaona kitu pekee cha kufanya ni yeye kukimbia tu.
Ndipo hapo alipoanza kukimbia bila kujua ni wapi anaelekea!, kivuli cha mafanikio ya Mbwana Samatta kianza kumtesa kuanzia hapo.
Alitamani kuyafanyia kwa vitendo yale maneno ambayo walikuwa wanayaongea wote wawili wakiwa TP Mazembe.
Kila alipokuwa anakumbuka kauli za kujipa moyo kati yao, kauli za kwamba kesho tunatakiwa kucheza ligi kubwa , kauli hizi zilikuwa zinamuumiza sana na ikizingatia anamuona mwenzake akiendelea kufanya vizuri katika ligi ya Ubelgiji.