Kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Adel Amrouche ametaja kikosi kitakachoingia kambini kujiandaa na michezo miwili yakufuzu Afcon Machi mwaka huu.
Adel Amrouche aliyetangazwa hivi karibuni kupewa mikoba ya Stars amewajumuisha wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi akichanganya na baadhi wanaocheza Ligi ya ndani.
Katika kikosi hicho yupo kiungo wa Yanga Feisal Salum “Fei Toto” ambae hajacheza muda mrefu na mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikua ni mwaka jana Disemba katika mchezo dhidi wa Yanga dhidi ya Polisi Tanzania.
Pia katika kikosi hicho cha Amrouche wanakosekana walinzi wa pembeni wa Simba Mohamed Hussein “Tshabalala” na Shomary Kapombe. Nafasi zao zimezibwa na Yahya Mbegu (Ihefu Fc) na David Luhende (Kagera Sugar).
Stars itakua na michezo miwili dhidi ya Uganda ambapo wataanzia ugenini nchini Misri Machi 27 halafu siku nne mbele watarudiana Benjamin Mkapa.