Timu ya Kijitonyama Combine imefanikiwa kulipa kisasi kwa kuichapa timu ya Chama la Wana Fc ambayo ni muunganiko wa wanafunzi waliosoma chuo cha St Augustine kwa mkoa wa Dar es alaam kwa mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa katika uwanja wa TTCL- Kijitonyama. Mchezo huo ambao ulikuwa ni wa kulipa kisasi kwa timu ya Kijitonyama Combine baada ya mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana katika viwanja vya Ardhi, kijitonyama ilikubali kulala kwa goli 2-1.
Mechi hiyo ambayo ilianza majira ya saa 11 za jioni, ikichezeshwa na David Chillo ” Wakili” ilianza kwa kasi ndogo huku timu zote zikishambuliana kwa zamu.
<<<Pakua app ya Spocha ikusaidie kutunza kumbukumbu za mechi zako na kuandaa ligi >>>
Iliwachukua dakika 37 pekee kwa timu ya Chama la Wana kuandika goli la kwanza kupitia kwa beki wa kulia Lusinde Julius kwa shuti kali la chinichini lililomshinda golikipa wa Kijitonyama Combine, Isamanyo. Goli hilo lilionekana kuwaamsha ushingizini timu ya Kijitonyama na kuanza kufanya mashambulizi ambapo dakika ya 41 walifanikiwa kusawazisha goli kupitia kwa mshambuliaji hatari Mgumo “Kagere” kwa njia ya penati baada ya Mgumo kufanyiwa rafu mbaya katika eneo la hatari.
Goli hilo lilionekana kuwa chachu kwa Kijitonyama Combine, kwani walionekana kutawala eneo la kati chini ya mchezaji fundi Juma J na Shaaban Mgomboro ambao walionesha kila dalili za kuwazidi viungo wa timu pinzani kwa kupiga pasi mpenyezo zilizoleta madhara kwa timu ya Chama la Wana. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu zote zilitoshana ubavu kwa kufungana goli 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya aina yake kwa timu zote mbili, huku Kijitonyama Combine ikifanya mabadiliko ya baadhi ya nyota wake kama Mgumo Kagere (Mfungaji wa goli la kwanza) Juma J, Mizengwe, na Isaya, nafasi zao zikichukuliwa na Shomari, Rama Kubwa na Mawazo na kwa upande wao Chama la Wana hakukuwa na mabadiliko yoyote.
Alikuwa ni Winga Mussa Masuke akiitanguliza timu ya Chama la Wana kwa kuifungia goli la kuongoza mapema katika dakika ya 50 kwa shuti kali lilimuacha golikipa asijue cha kufanya baada ya mabeki wa Kijitonyama Combine wakidhani kuwa mfungaji alikuwa amekwisha otea.
Baada ya goli hilo la kuongozwa Kijitonyama Combine alionekana kujitahidi kurudi mchezoni kwa kushambulia kwa kupitia pembeni ambapo katika dakika ya 53 Kijitonyama Combine ilisawazisha goli kupitia kwa winga msumbufu Mawazo baada ya golikipa wa Chama la Wana , Ibrahim Kapona kuchelewa kuukoa mpira ikiwa ni pasi mpenyezo kutoka kwa Rama Kubwa.
Baada ya magoli hayo kufungwa huku dakika zikiwa zinayoyoma, mpira ulionekana kuongezeka kasi na timu zote zilianza kutumia nguvu katika kuhakikisha ushindi unapatikana.
Timu zote zilishambuliana lakini Kijitonyama Combine ilionekana kuwa vizuri zaidi kwani ndio waliokuwa wakifika langoni kwa wapinzani wao mara kwa mara. Dakika ya 76 Kijitonyama Combine ilijiandikia goli lake la tatu kupitia kwa beki wake wa kulia Roja kwa kichwa safi kilichojaa kimyani huku golikipa akiwa ameshatoka golini.
Baada ya goli hilo, Kijitonyama Combine ilikosa nafasi nyingi za wazi kupitia kwa washumbuliaji wa pembeni wakiongozwa na Mawazo ambaye ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa timu ya Chama la wana. Hadi filimbi ya mwisho inapulizwa, Chama la Wana Fc imekubali kulala kwa goli 3-2.
Baada ya mchezo huo, nahodha wa Chama la Wana Fc, Lusinde Julius amesema kuwa wamekubali kipigo hicho na watajipanga kwa mechi zijazo.
” ilikuwa ni mechi ya kirafiki na walitupania sana kwani walitaka kulipa kisasi na wamefanikiwa, sisi kama timu tutajipanga kuhakikisha mechi zijazo tunapata matokeo mazuri”
Na upande wake Mfungaji wa goli la pili kwa timu ya Kijitonyama Combine, Mawazo amesema kuwa wao kama timu wanafurahi kulipa kisasi
” kwanza tuna furaha baada ya kuwafunga maana tumefanya mazoezi ya kutosha hivyo tungejisikia vibaya kama tungefungwa”
“mchezo huu kwetu unatuandaa zaidi maana Jumatano tutakuwa uwanjani katika mashindano ya kumgombania mbuzi na nina imamni tutashinda pia, hivyo nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutushangilia nasi hatuta waangusha”
Katika mchezo huo timu ya Kijitonyama Combine ilifanya mabadiliko kwa wachezaji zaidi ya wanne, lakini timu ya Chama la wana haikufanya mabadiliko yoyote ndani ya dakika zote tisini.