ACHANA na nafasi ya wazi aliyopoteza kwa kushindwa kutulia na kufunga kwa kichwa mwanzoni mwa kipindi cha kwanza katika mchezo wa ‘Dar es Salaam-Pacha’ siku ya Jumapili iliyopita, winga wa Simba SC, Shiza Kichuya anapaswa kujitazama upya kiuchezaji ili asiendeleee kuporomoka.
Kwa dakika 62 za mchezo wa ligi kuu dhidi ya mahasimu wao Yanga SC, Shiza si tu hakuwa na madhara kwa wapinzani wake bali ameendelea kuonyesha anatakiwa kukaa benchi na kumpisha Hassan Dilunga ama Mohamed Ibrahim ambaye alimbadili Shiza na kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo uliomalizika kwa suluhu-tasa.
KUACHWA TIMU YA TAIFA
TIMU YA Taifa siku zote huwapandisha thamani wachezaji, na baada ya miaka miwili na nusu akiitwaa bila kukosekana katika kikosi cha Taifa Stars, Shiza ametupwa nje ya kikosi kwa mara ya kwanza na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike.
Stars ilicheza bila Shiza katika mchezo uliopita wa kufuzu CAN 2019 dhidi ya majirani zetu Uganda na mfumo wa Amunike ambao alimtumia zaidi mlinzi wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael kupandisha timu akitokea upande wa kushoto ukaficha kabisa nafasi ya Shiza na wala hakukuwa na pengo lolote katika mchezo uliomalizika kwa suluhu-ta pale Kampala.
Shiza alikosekana kutokana na makosa ya kinidhamu ‘waliyobambikiwa’ lakini baada ya mwezi mmoja na jina lake halikutajwa kabisa katika orodha ya wachezaji 30 ambao wanajiandaa na mchezo dhidi ya Visiwa vya Cape Verde Oktoba 10. Hakuna shaka, ameachwa kutokana na kiwango chake cha chini klabuni Simba.
AMESHUKA KIWANGO
Katika mchezo dhidi ya Mbao FC 1-0 Simba, Mwadui FC 1-3 Simba kiwango cha kumiliki mpira na upigaji wa pasi cha Shiza kilikuwa na mashaka makubwa. Si, Kichuya yule ambaye alikuwa akikimbia akitazama juu mpira ukiwa mguu mwake, si Shiza yule ambaye alikuwa akivamia lango la wapinzani kwa kasi na kupiga mashuti goli, na katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga kiungo huyo wa pembeni alionyesha wazi amepoteza kujiamini na si yule ambaye alijitambulisha katika soka la Tanzania kwa goli maridadi la kona ya moja kwa moja katika mchezo dhidi ya Yanga misimu miwili iliyopita.
Yote ni kutokana na kushuka kwa kiwango chake kiuchezaji, kujiamini, na inavyoonekana kupoteza nafasi kadhaa za wazi Jumapili iliyopita ‘kutammaliza’ zaidi ikiwa atashindwa kusaidiwa. Naamini, Shiza anajitazama kama mchezaji ‘asiyethaminiwa’ baada ya kuachwa Stars jambo linaloweza kumuingiza katika ‘msongo’ wa mawazo na mara moja au mbili akianza kuwekwa benchi Simba si ajabu kitamkuta kilichomkuta Muzamiru Yassin.
Kama mwanasoka, Shiza anatakiwa kukubali ukweli kuwa sasa yupo nje ya kikosi na yupo hatarini kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Simba kama ataendelea kucheza kwa kupoteza hovyo mpira na upigaji wa pasi nyingi zisizofika.
Shiza ni kijana anayejituma, na mwenye ndoto kubwa kimpira hivyo anapaswa kuelewa baada ya misimu miwili mizuri Mtibwa Sugar FC, mingine mizuri Simba msimu wake huu wa tano ligi kuu atakutana na changamoto nyingi kiuchezaji-kushuka na kupanda kwa kiwamgo chake hivyo anapaswa kuonyesha ukomavu zaidi.
AKUBALI KUCHEZA ANAVYOTAKA MWALIMU
Kitu kipya kilichompaisha Shiza katika soka la Tanzania ni kufunga goli la kona ya moja kwa moja katika pambano la mahasimu wa soka nchini, ndiye pekee katika karne hii ya 21, na aliendelea kufunga mara tatu mfullizo katika mchezo wa ‘Dar-Pacha’ hivy kuungana na Mrundi, Amis Tambwe kama wachezaji pekee kufunga mfululizo mara tatu katika Yanga v Simba.
Kufanya kwake kitu kipya katika ‘Pacha’ hiyo ya tano kwa ubora Afrika kulimpa umaarufu mkubwa Shiza labda hili ndiyo lilipelekea kumgomea kocha Masoud Djuma msimu uliopita alipotaka kumtumia kama wing-back wa kushoto. Tatizo mojawapo kubwa linalofanya baadhi ya wachezaji kupoteza ubora na nafasi zao kikosini ni kushindwa kucheza vile anavyotaka mwalimu. Soka la sasa licha ya kwamba wachezaji wanatumia vipaji na maarifa yao binafsi lakini mbinu za kimchezo lazima ziwe msimu na katika hili kocha na timu yake ya ufundi uchagua wachezaji wa kuwatumia katika mechi kutokana na mbinu wanazotaka kuzitumia.
Kichuya kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa Kitanzania si wepesi wa kucheza kwa kufuata mbinu za walimu, yeye anaamini zaidi katika kipaji chake, ndiyo, lakini tazama kipaji chake hicho cha kupiga pasi ndefu za mwisho za kupenyeza kilimsaidia lolote katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga? Alipiga pasi nzuri lakini sehemu ambazo wenzake hawakuwepo.
Hili afanikiwe kabla ya kupelekwa benchi ni lazima sasa akubali kucheza kwa kufuata maelekezo ya makocha wake hata kama atakuwa na maarifa yake binafsi kiuchezaji. Asipobadilika sasa atakuwa sawa na ile ngoma ivumayo sana ambayo mwisho wake upasuka, sababu alishafanya kitu kipya katika Dar-Pacha ndiyo maana ni maarufu hadi sasa.