Kevin Kongwe Sabato “Kevi Kiduku” katika msimu uliopita alimaliza Ligi akiwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro huku akiwa ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika kikosi cha Zubeiry Katwila kabla ya kuamua kuachana nayo katika msimu huu wa 2019/2020.
Kevin Kiduku mchezaji wa zamani wa Abajalo Fc ya Sinza alipata nafasi katikati ya msimu uliopita ya kwenda katika majaribio nchini Afrika Kusini. Klabu yake ya Mtibwa Sugsr ilimpa baraka zote lakini hakufanikiwa kupata nafasi nchini humo na hivyo kuamua kurudi nchini na kuendelea kuitumikia klabu yake hiyo.
Dirisha kubwa la usajili lilipofunguliwa Kevin Sabato alikua ni miongoni mwa nyota walionaswa na matajiri wa Mwanza Gwambina fc iliyopo Ligi Daraja la kwanza ili kwenda kuipandisha timu hiyo mpaka Ligi kuu.
Baada ya usajili huo mashabiki wengi wa soka walibaki na maswali ni kwanini Kevi Kiduku ameamua kwenda kutumikia katika timu ya Ligi Daraja la kwanza na kuamua kuachana na kucheza Ligi Luu ambapo baadhi ya timu zilikua zinataka huduma yake.
Lakini baada ya kuitumikia Gwambina nusu msimu tuu aliamua kutimka zake na kujiunga na Kagera Sugar chini ya mwalimu Mecky Mexime na kurudisha makali yake ya kufumania nyavu kama kawaida. Huku sababu kubwa iliyomtoa Gwambina ikisemekana na kutokuelewana na kocha wake Novaty Fulgence.
Tangu ajiunge na Kagera Sugar Kevin Sabato amefunga jumla ya mabao 6 ikiwemo “Hatrick” dhidi ya Singida United huku pia akifanikiwa kuibuka Galacha wa mabao kwa mwezi Februari baada ya kufunga mabao matano na kuwagalaza Reli Lusajo wa Namungo na David Richard wa Alliance.