Sambaza....

Mtandao wako wa kandanda.co.tz umekuwekea kanuni za Ligi Kuu Tanzania 2023. Hii ni sura ya kwanza (1) kanuni namba 1. Ambayo inazungumza kuhusu Uchezaji wa kiuungwana.

1: Cheza Kiungwana

Ushindi hauwezi kuwa na thamani iwapo umepatikana katika njia isiyo halali au kwa udanganyifu. Kudanganya ni rahisi lakini haileti raha ya ushindi. Kucheza kiungwana inahitaji moyo na tabia njema. Pia hufurahisha zaidi. Mchezo wa kiungwana siku zote una malipo yake hata kama utapoteza mchezo. Kucheza kiungwana kunakujengea heshima wakati kudanganya kunaleta aibu. Kumbuka kuwa mpira wa miguu ni mchezo na mchezo wowote hauwezi kuwa na maana kama hautochezwa kiungwana kwa kuzingatia kanuni na taratibu ili mshindi halali aweze kupatikana

2: Tafuta Ushindi, Kubali Kushindwa

Kushinda ndiyo lengo la kushiriki katika mchezo wowote ule. Siku zote usijiandae kushindwa. Iwapo uchezi kwa nia ya kushinda utakuwa unawadanganya wapinzani wako, unawadhulumu watazamaji na pia unajifanya mwenyewe kuwa ni mjinga. Usikate tamaa hata siku moja unapopambana na wapinzani wenye
nguvu zaidi lakini pia usidharau hata siku moja unapopambana na wapinzani dhaifu.
Ni kumkosea adabu mpinzani unapocheza chini ya kiwango chako. Cheza kwa nia ya kutafuta ushindi hadi dakika ya mwisho lakini kumbuka hakuna anayeshinda wakati wote. Siku nyingine utashinda na
siku nyingine utashindwa. Jifunze kukubali kushindwa. Usitafute visingizio unapofungwa. Sababu za kweli siku zote zitadhihirika. Wapongeze washindi bila kinyongo. Usilaumu waamuzi wala mtu mwingine yoyote. Jizatiti kufanya vizuri zaidi wakati mwingine. Walioshindwa na kukubali wanapata heshima zaidi uliko washindi wanaolazimisha.

3: Heshimu Sheria za Soka

Michezo yote inalindwa na sheria. Bila sheria itakuwa ni vurugu tupu. Sheria za mpira wa miguu ni nyepesi na rahisi kujifunza. Hakikisha unajifunza; itakusaidia kuufahamu mpira wa miguu vizuri zaidi. Kuufahamu chezo zaidi itakufanya uwe mchezaji bora zaidi. Pia ni muhimu kufahamu madhumuni ya sheria zilizowekwa. Zimekusudiwa kuufanya mchezo uwe na ladha katika kuucheza na kuuangalia. Kwa kufuata sheria, mchezo wa mpira wa miguu utakuwa na burudani zaidi.

4: Heshima kwa Wote

Mchezo wa kiungwana unamaanisha kuheshimu wapinzani. Bila ya wapinzani kutakuwa hakuna mchezo. Kila mmoja ana haki sawa, ikiwemo haki ya kuheshimiwa. Wachezaji wa timu moja ni wenza. Tengeneza timu ambayo kila mmoja kwenye timu atakuwa na haki sawa. Waamuzi wapo kuhakikisha nidhamu na mchezo wa kiungwana unadumishwa. Siku zote kubali maamuzi yao bila ya ulalamishi, na wasaidie waweze kuwafanya washiriki wote waufurahie zaidi mchezo. Viongozi pia ni sehemu ya mchezo na anatakiwa wapewe heshima wanayostahili.
Watazamaji wanaufanya mchezo uwe na msisimko. Wanahitaji kuuona mchezo ukichezwa kiungwana kwa kuzingatia kanuni, lakini pia wanatakiwa kuwa waungwana na kujiheshimu.

5: Dumisha Maslahi ya Mpira

Mpira wa miguu ndiyo mchezo unaoongoza duniani. Lakini siku zote unahitaji msaada wa kila mmoja uufanya uendelee kuwa mchezo wenye kupendwa zaidi. Fikiria maslahi ya mpira kabla ya maslahi yako
mwenyewe. Fikiria ni vipi vitendo vyako vinaweza vikaupaka matope mchezo wa mpira wa miguu. Zungumzia mambo mazuri ya mchezo wa mpira wa miguu. Shawishi watu wengine kuuangalia na kuucheza kiungwana. Wasaidie wengine kupata burudani ya kutosha katika mchezo wa mpira wa miguu kama unayoipata wewe. Kuwa balozi wa mchezo wa mpira.

6: Heshimu wanaolinda Heshima

Jina zuri la mchezo wa mpira wa miguu limeendelea kudumu kwa sababu idadi kubwa ya watu wenye kuupenda mchezo huu ni wakweli na waungwana. Wakati mwingine mtu hufanya jambo kubwa ambalo linastahili tulitambue. Watu kama hawa wanastahili kutuzwa na mambo mema waliyofanya yatangazwe. Hii itashawishi wengine kuiga mifano yao. Saidia kuendeleza mpira wa miguu kwa kuyatangaza mazuri yake.

7: Kataa Mambo yote ya Hatari

Umaarufu mkubwa wa mchezo wa mpira wa miguu wakati mwingine huufanya uwe rahisi kuathiriwa na mambo mabaya ya nje. Jichunge na vishawishi vitakavyokufanya ushawishike kushiriki kwenye kudanganya au kutumia madawa yaliyokatazwa. Madawa yaliyokatazwa hayana nafasi katika soka, mchezo mwingine wowote na jamii kwa jumla. Sema hapana kwa madawa ya kulevya. Saidia kuupiga teke ubaguzi kwenye soka.
Wachukulie wachezaji wote na wengineo kuwa ni sawa bila kujali dini zao, kabila, jinsia au utaifa wao.
Usivumilie hata kidogo kamari katika michezo unayoshiriki. Inaporomosha kiwango chako cha uchezaji na inasababisha hali ya mgongano wa maslahi. Thibitisha kuwa soka haihitaji fujo, hata kutoka kwa washabiki wako wenyewe. Soka ni mchezo na michezo huleta amani.

8: Wasaidie Wengine Kupambana

Wakati mwingine unaweza kusikia wachezaji wenzako au watu wengine unaowafahamu wanashawishiwa wadanganye kwa njia moja au nyingine au washiriki katika vitendo visivyokubalika katika mchezo wa soka.
Wanahitaji msaada wako. Usisite kusimama upande wao. Wape nguvu ya kukataa vishawishi. Wakumbushe wajibu wao kwa wenzao na kwa mchezo wenyewe. Tengeneza umoja wenye mshikamano, kama ngome ngumu kabisa kwenye mchezo wa soka.

9: Waibainishe Wachafuzi

Usione aibu kusimama dhidi ya yoyote yule ambayeuna hakika anashawishi wengine kudanganya au kushiriki katika vitendo vingine visivyokubalika. Ni vyema kuwafichua
waovu wote ili waweze kuondolewa kabla ya kuleta madhara. Ni uovu kushirikiana na watu waovu. Usiseme tu hapana, wafichue wanaotaka kuichafua soka kabla hawajafanikiwa kuwashawishi wengine.

10: Soka Kujenga Dunia Bora zaidi

Soka ina nguvu ya ajabu inayoweza kutumika kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi. Tumia nguvu hii kudumisha amani, usawa, afya na elimu. Ifanye soka iwe bora zaidi, ipeleke kwa jamii kujenga dunia bora zaidi.

Wachezaji pia Wanawajibika Kuzingatia na kudumisha

(a) Nidhamu

Kudumisha tabia njema nje ya uwanja na wakati wote wa mchezo kwa kucheza bila ya kuwaumiza au kuhatarisha usalama wa wachezaji wa timu pinzani.

(b) Mchezo wa Kiungwana

Kutodanganya kuumia au kufanyiwa rafu, kutotumia mbinu zisizo za kiungwana mchezoni au kujiingiza katika vitendo visivyokuwa vya kiuanamichezo kama vile kutukana kwa maneno, ishara au kujihusisha na vitendo vyovyote vya kibaguzi.

(c) Kutorejeshea

Kutorejeshea (retaliation) iwapo mchezaji atafanyiwa rafu au kukashifiwa.

(d) Malalamiko

Mchezaji wakati wote anatakiwa atii maagizo ya kocha wake. Mchezaji anatakiwa akubali kubadilishwa uwanjani na kuadhibiwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu au visivyokuwa vya kiuanamichezo.
Ni nahodha pekee anaruhusiwa kuzungumza na waamuzi. Iwapo patatokea malamiko yoyote wakati wa mchezo wachezaji wengine wote wanatakiwa wawe hatua zisizopungua kumi kutoka kwa mwamuzi.

(f) Kuheshimu Nahodha

Mchezaji anatakiwa amheshimu na atii maagizo ya nahodha wake nje na ndani ya uwanja hususan katika masuala yahusuyo timu na tabia njema kwa jumla.

(g) Kuheshimu Wachezaji

Mchezaji awaheshimu wachezaji wenzake, awatie hamasa nje na ndani ya uwanja. asimkashifu mchezaji mwenzake mwenye kufanya makosa.

(h) Kuheshimu Wapinzani

Mchezaji awape wachezaji wa timu pinzani heshima yao, awe tayari kutoa msaada kwa mchezaji aliyeumia na kushikana mikono kabla na baada ya mchezo.

(i) Kuheshimu Waamuzi

Mchezaji anatakiwa wakati wote kuheshimu maamuzi ya waamuzi na kutozozana nao au kutumia lugha ya matusi au kashfa dhidi yao.

(j) Kujiheshimu Mwenyewe

Mchezaji anatakiwa ajiheshimu mwenyewe na ajitunze na asitumie madawa yaliyokatazwa

Tujadili katika eneo la gumzo hapo chini, Kanuni hizi zinaiweka katika taswira gani ligi yetu na ulimwengu wa kandanda. Tunaendelea kuweka kanuni zaidi.

Sambaza....