Sambaza....

Kiungo wa Yanga Sc,  Mzimbabwe Thabani  Scara Michael Kamusoko leo amewaaga rasmi  wadau wa soka nchini, wapenzi na mashabiki wa klabu ya Yanga.

Kamusoka ambaye anafahamika zaidi kama mchezaji wa kiungo cha kati mwenye umahiri mkubwa wa kupiga pasi, kumiliki mpira na kupiga mashuti ya haja anapopata upenyo wa kufanya hivyo.

Mzimbabwe huyo ameitumikia yanga tangu msimu wa mwaka 2015/2016, alisajiliwa Julai 1, 2015 akitokea FC Platinum kwa mkataba wa miaka miwili. July 2017 Kamusoko aliongeza mkataba na mabingwa hao wa kihistoria wa miaka miwili.

Kiungo huyo mwenye miaka 30, leo kupitia ukurasa wake wa kijamii, ameandika hivi “ kipindi chote nilipokuwa hapa Yanga, nilijifunza vitu vingi, nilikuja hapa Yanga na kujifunza jinsi gani watu watakukubali na kukupongeza unapoonesha juhudi na kujituma kwa ajili ya klabu, naweza kusema, nawashukuru sana mashabiki na watu wote kwa upendo mlionionyesha na bado mnauonyesha, nauthamini sana upendo wenu, ASANTENI SANA”.

Akiwa na Lwandamina

Kamusoko hadi sasa, amefanikiwa kunyanyua kwapa, mara tatu akiwa na klabu ya Yanga. Amebeba mataji mawili ya Ligi kuu Tanzania bara msimu wa mwaka  2015/16 na 2016/17. Amefanikiwa pia kubeba kombe la shirikisho lijulikanalo kama Azam Sports Federation Cup mara moja msimu wa mwaka 2015/16.

Kamusoko ameisaidia Yanga katika mechi za kitaifa na hata kimataifa, mbali na kuisaidia klabu yake hiyo kubeba mataji hayo matatu tangu ajiunge nao mwaka 2015, lakini pia ameiwezesha Yanga kufuzu katika hatua ya makundi katika mashindano ya Shirikisho Afrika mwaka 2016 na 2018.

Kamusoko na Ngoma

Miongoni mwa vitu ambavyo  vitanifanya nimkumbuke Kamusoko ni staili yake ya maisha kama kiongozi kwa wachezaji wengine ndani na hata nje ya Uwanja. Ni mara nyingi alikuwa akipewa majukumu ya kuwa nahodha katika mechi mbalimbali za ligi. Pia nakumbuka alishawahi kuwa nahodha msaidizi akisaidiana na Juma Abdul katika nafasi hiyo huku nahodha mkuu akiwa Nadir Haroub Ally “Cannavaro” na kisha Kelvin Yondan.

Haitokuchukua hata sekunde 10 kumtambua kiungo huyo hundi awapo uwanjani hasa kutokana na staili yake ya uchezaji na hata staili ya nywele zake.

Kikubwa pia ninachokikumbuka kwake ni ufundi katika kupiga penati. Unaikumbuka penati aliyomfunga Aishi Manula katika mchezo wa ngao ya jamii, mwaka 2017? “PANENKA PENALTY GOAL” licha ya Simba kuibuka na ushindi lakini penati ya fundi huyo ilionekana kuwa bamba wengi na hata mashabiki wa Simba wenyewe. Je wewe unamkumbuka Kamusoko kwa tukio gani nje na hata ndani ya uwanja?

Sambaza....