Wekundu wa Msimbazi Simba wakiwa ugenini wamekubali kichapo cha mabao matatu kwa moja mbele ya Raja Casablanca katika mchezo wa mwisho wa kundi C wa Ligi ya Mabingwa Afrika na hivyo kupoteza rekodi yake ya muda mrefu ya kutokufungwa nje ndani na wapinzani wake.
Mambo yapo hivi, tangu mwaka 2003 klabu ya Simba imekua ikipata matokeo mazuri mbele ya vigogo wa Afrika katika mchezo mmoja kati ya miwili ambayo hukutana katika Ligi ya Mabingwa. Simba imekua ikipata ushindi ama sare katika michezo miwili ambayo hushuka dimbani dhidi ya timu yoyote wanayokutana nayo hivyo matokeo ya kufungwa na Raja ugenini yamevunja rekodi yao.
Mchezo wa kwanza uliopigwa Jijini Dar es salaam Simba walikubali kipigo cha mabao matatu kwa bila mbele ya mashabiki wake na katika mchezo wa leo pia wamekubali kipigo cha mabao matatu kwa moja ugenini katika Jiji la Casablanca.
Mchezo Wenyewe Ulivyokua!
Simba walianza vyema katika kipindi cha kwanza licha ya mashambulizi mengi na kasi kubwa ya Raja lakini walifanikiwa kuwazuia washambuliaji wa Raja Casablanca kabla ya Joash Onyango kufanya makosa na kupelekea Hamza Khaba kuandika bao la kwanza dakika ya 44.
Kipindi cha pili Simba ilirudi vizuri na kuandika bao dakika ya 48 kupitia kwa Jean Baleke aliyefunga kwa ustadi mkubwa akipokea pasi nzuri kutoka kwa Mzamiru Yasin. Raja waliongeza goli la pili tena kwa mkwaju wa penati baada ya Onyango tena kufanya makosa ndani ya eneo la hatari na Hamza Khaba tena akafunga bao la pili. Bao la tatu la Raja lilifungwa dakika ya B. Mohamed katika dakika ya 86 ya mchezo.
Licha ya kufungwa katika mchezo huo lakini tayari Simba ilishafuzu na kusonga mbele kwenda robo fainali kwani tayari walishakusanya alama 9 mbele ya Horoya (7) na Vipers wenye alama 2.