Hatimae mwezi wa mahaba mwezi wa pili umemalizika na mwezi wa tatu umeingia ikiwa leo ni March mosi ya mwaka 2023. Katika soka mwezi huu umebeba hatma kubwa kwa vilabu vyetu vikongwe hapa nchini Simba na Yanga.
Katika mwezi March kupitia mitandao yao yakijamii tayari vilabi hivyo vimetoa ratiba zao ambapo kila timu itashuka dimbani mara nne. Lakini pia kutakua na mapumziko kupisha michezo ya Kimataifa na timu yetu ya Taifa “Taifa Stars” itashuka dimbani dhidi ya Uganda.
Simba wao watakua na michezo minne mmoja ukiwa wa kombe la FA na mmoja wa Ligi Kuu ya NBC halafu watakua na michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika michezo hiyo ni mmoja pekee watakua ugenini.
Simba wataanzia nyumbani March mbili dhidi ya African Sports ya Tanga katika kombe la FA mchezo utakaopigwa uwanja wa Uhuru. Halafu March saba watawakaribisha Vipers ya Uganda Benjamin Mkapa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa kisha watakwenda ugenini kuvaana na Mtibwa Sugar kwenye Ligi Kuu ya NBC. Simba wataimaliza March kwa mchezo mwingine wa nyumbani wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Horoya kutoka Guinea.
Yanga wao watacheza michezo yote minne nyumbani na kazi itaanza March tatu watakapowakaribisha Tanzania Prisons katika kombe la FA ambalo wao ndio mabingwa watetezi, halafu watarudi katika anga la Kimataifa kwa kuwakaribisha Real Bamako kwenye Kombe la Shirikisho. Yanga watakutana na kibarua kingine katika Ligi kwa kuwakaribisha Geita Gold kabla ya kumalizia mwezi na US Monastir kwenye mchezo wa Kundi D Shirikisho Afrika.
Baada ya vigogo hao kumaliza ratiba zao tarehe 18 na 19 ya mwezi wa tatu watapumzika na kuipisha timu ya Taifa ya Tanzania kucheza michezo yake ya kufuzu Afcon.