Kwa kumbukumbu zangu za haraka haraka najaribu kuangalia namna hayati Mzee AE Musiba alivyoweza kutuaminisha kwamba Willy Gamba ni mwanadamu anayeishi na asiyeshindwa katika mpango wowote,hasa katika kitabu cha Kikosi cha Kisasi.. ungeona namna ambavyo Gamba angepokea maelekezo kutoka kwa Chief kupitia kwa Maselina, halafu yeye akajiongeza kwa mbinu zake tofauti kabisa na kumaliza operesheni yeyote atakayotumwa..
Najaribu kuufananisha ufanisi wa Liverpool ya meneja Jurgen Norbet Klopp na System ya Chief kwenda kwa Willy Gamba na matokeo wanayopata,
Je ni sahihi kwa Liverpool kuendelea na mfumo wanaotumia?
Kwa Misimu si chini ya minne sasa, Jurgen Klopp alikua anatengeneza jiko lake la tofauti akipika mfumo anaouabudu na pengine anaofikiri utampa mafanikio.. Akichezesha timu yake kwa kasi na kwa mibadilishano ya haraka huku wakikaba kwa kasi kuanzia juu mbele ya kiwanja na kwa vikundi mara mpira unapopotea. Staili hii iliyobatizwa jina la GenGen Pressing imekua ikitabiriwa kila msimu mmoja unapoisha na wengi wa umma wa wapenda Soka kuwa itawachosha na kuwaletea majeruhi wachezaji na kisha kuwa na mafanikio ya msimu mmoja.
Matokeo yake yamekua hua ni mafanikio mapya kila msimu mpya unapokuja. Hii ni kwa nini, na je Klopp alianzaje na amefanikiwa namna gani?
Klopp alianza pale Liverpool akiwaambia washabiki wake kuwa anataka wabadilike kutoka kuwa wenye wasiwasi na kuwa waamini (from Doubters to Believers) na kisha akaanza na kikosi alichokikuta huku akiingiza maingizo yake taratibu. Jaribio la la kwanza ikawa kufungwa fainali ya Kombe la Ligi na Mannchester City kwa penati, Kisha msimu unaofuata akafungwa Fainali ya Kombe la Europa na Seville ya Hispania, na mwaka mmoja baadae akafungwa na Real Madrid kwenye Fainali ya UEFA Chapmions League. Hii ilifuatiwa na miaka miwili yenye mafanikio kwao Liverpool. Wakibeba UEFA Champions League, na kisha UEFA Super Cup, FIFA kombe la Dunia la Vilabu na hatimaye ubingwa wa Uingereza.
Kwa harakaharaka hii ni mfano hai wa namna chakula kinachopikwa hupokelewaje na walaji baada ya wapishi kuzoea kazi kutoka kwa mpishi mkuu.
Liverpool kwa miaka hii mitatu wamekua wakicheza kwa kutumia viungo watatu ambao wote kazi yao kubwa wanayotumwa si Ubunifu bali kuwa watumwa. Kazi yao kubwa ni kuhakikisha kuwa mabeki wawili wa pembeni wanakuwa na nafasi ya kubadilishana mipira kwa haraka (hii inawahitaji watu wenye utimamu wa kufanya hivyo) na kuwa na madhara makubwa kutokea pembeni na kuwafanya wale wachezaji wao watatu wa mbele wawe na madhara mara mbili zaidi.
Katika mfumo huu wale watatu wa mbele pia wanakua na kazi kubwa ya kuhakikisha wanasaidia kwa haraka pande zote mbili za mabeki wao wa pembeni endapo mipira itanyang’anywa wakishirikiana na watatu wa katikati.
Hapa utagundua kwanini Andy Robertson na Trent Alex Anord wanakua wana madhara makubwa sana kwa wapinzani wao na kisha Sadio Mane, Mo Salah na Roberto Firmino. Hii ni kwa sababu kazi chafu wanazofanya Gini Wijnaldum, Henderson na Fabinho zinaonekana kwa shida sana. Hawa ni watu muhimu kwa ufanisi kwenye ubadilikaji wa haraka (quick transistion) hawatakiwi kua na mambo mengi zaidi ya UFANISI mkubwa.
Hili inawahusu hata mabeki wao wa kati wakiongozwa na Virgil Van Dijk. Ndio maana Liverpool wakikukaba kwa nguvu ukipoteza mpira, kama timu yako inaweza kukaba nayo kwa haraka basi iaze na kumkaba Van Dijk, Trent na Robertson. Hawa ni watu muhimu kwenye mwanzo wa magoli mengi ya Liverpool huku wakifanyiwa kazi nzito na wale viungo watatu.
Swali linakuja, Je Liverpool wataweza kuendelea kutesa timu nyingine kwa mfumo huu huu ndani ya mwaka wa nne sasa? Je makocha pinzani hawajsoma Jurgen Klopp?
Sitaki kuwa mtabiri ila nimeiangalia Liverpool ikicheza mechi tatu za Pre Season, Ngao ya Jamii na mechi ya ufunguzi wa Ligi. Namuona Klopp akiendelea ma mfumo huu huu anaoupenda ila tu ataendelea kuufanyia maboresho tu.
Kucheza kiungo mbunifu ila anayekaba kwa kunusa maeneo yenye hatari (track back), hii yaweza kua ni sababu kubwa ya kumsajili Thiago Alcantara kutoka FCB ya Ujerumani. Lakini pia kutakua na kuendelea kutumia pia mshambuliaji anayekaba kwa njia hiyo (Sababu Kubwa ya Firmino Kubatizwa Jina la Mshambuliaji Mkabaji) na nahisi ndio sababu kubwa ya kusikia Liverpool wanamtaka kijana wa Wolves Diogo Jota
kkuna kipya Liverpool chini ya Klopp wanapika? Jibu litapatikana uwanjani.
Willy Gamba hakuwahi kufeli kwenye operesheni zote alizotumwa na Chief. Kuanzia Kikomo, Kikosi cha Kisasi, Kufa na Kupona, Hofu na Kisha Njama, Operesheni zote hizo alizitoboa. Je Klopp ataweza kwenda mwaka wa nne na mbinu zilezile? au Ndio wapinzani wameshamsoma?
Ligi imerudi Kwetu tuandae Ubongo na Macho kuweza kuona mipambano ya mbinu miongoni mwa waalimu wabobezi wa Ligi hii pendwa!
Jackson Kulanga, katuandikia kupita “Tuandikie Usomwe“