Sambaza....

KUMSAINI, Thomas Ulimwengu kama nyongeza katika safu ya mashambulizi ni ´kamari´ itakayowagharimu sana Simba SC kama malengo yao ni kufanya vizuri katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika 2018/19.

Wakati wa usajili wa dirisha kubwa katikati ya mwaka huu, Simba iliwasaini washambuliaji wanne wapya. Marcel Kaheza ambaye alifunga magoli 15 katika ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita akiichezea Majimaji FC, Mohamed Rashid aliyefunga magoli 12 wakati akiichezea Tanzania Prisons, Adam Salamba aliyefunga magoli nane wakati akiichezea Lipuli FC.

Usajili huo ulianza kuonyesha dalili mbaya katika michuano ya SportPesa Super Cup iliyofanyika Nakuru, Kenya mwezi Juni. Baada ya michezo mitatu pasipo kufunga Simba ilimsaini mfungaji bora wa michuano hiyo Mnyarwanda, Meddie Kagere ambaye aliwafunga moja ya magoli mawili yaliyoipa Gor Mahia FC ushindi wa 2-0 katika mchezo wa fainali.

USAJILI WA KUKOMOANA.

Washambuliaji wote hao wanne walisajiliwa bila kushirikishwa makocha Mfaransa, Pierre Lechantre na Mrundi, Masoud Djuma ambao ndio walikuwepo wakati wachezaji hao wakisajiliwa.

Kagere

Salamba, Kaheza, Rashid na Kagere wote hao walihitajika kwanza Yanga lakini Simba kwakuwa walikuwa na cash haraka wakaingilia dili zote hizo na kuwasaini. Niliandika wakati ule kuwa haukuwa usajili stahili kwao nadhani miezi minne sasa ukitoa Meddie aliyefunga magoli saba katika ligi kuu na mengine manne katika Cecafa Kagame Cup, Salamba, Kaheza na Rashid hawajafanya kipya chochote hadi sasa.

TUYISENGE SI ULIMWENGU

Kwa aina ya kikosi walichonacho na michuano iliyo mbele yao, naelewa kwanini kocha Mbelgiji, Patrick Aussems anahitaji nyongeza ya mshambulizi licha ya uwepo wa nadhodha John Bocco na Mganda, Emmanuel Okwi ambao kwa pamoja walifunga jumla ya magoli 34 katika ligi kuu msimu uliopita.

Aussems anahitaji mfungaji wa ziada lakini si kama Ulimwengu ambaye kwa miaka mitatu amecheza chini ya michezo 30 katika klabu na timu ya Taifa kutokana na majeraha ya goti. Tom alisaini Al Hilal ya Sudan- klabu kubwa tajiri na yenye mafanikio zaidi Sudan, lakini wameamua kuachana nae kutokana na majeraha.

Ulimwengu

January 2017, Tom alisaini mkataba wa miaka miwili kuichezea AFC ya Sweden, lakini kufikia mwezi Disemba, 2017 alikuwa amecheza mchezo mmoja tu kutokana na majeraha. Waswiden hao wakavunja mkataba wake. Anapokuwa timamu kimwili, Tom ni mchezaji mkali, lakini Simba watafanya makosa makubwa kama watamsaini.

Mnyarwanda, Jacques Jakaka Tuyisenga yupo fiti kimwili na kiakili, ni mfungaji namba moja wa Gor Mahia. Tuyisenga hucheza pamoja na Meddie katika safu ya mashambulizi ya timu ya Taifa ya Rwanda, pia walikuwa washambuliaji-pacha katika kikosi cha Gor. Ili kumsaidia kwa dhati Aussems ni bora uongozi umsaini Jakaka kuliko Tom.

Tuyisenge ni silaha ya uhakika kuliko Tom ambaye ni nadra sana kwake kucheza michezo saba-kumi mfululizo pasipo maumivu. Ulimwengu ni kamari na haitakuwa na matokeo mazuri. Ili kushindana Afrika Simba ni lazima waachane na sajili za wasiwasi.

Sambaza....