Rais wa Yanga Hersi Ally Said amevunja ukimya wake kuhusu kocha wa klabu hiyo Nasreddine Nabi anayehusishwa na Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini.
FAR Post imeripoti kuwa Nabi yuko katikati ya mazungumzo na Kaizer Chiefs kuchukua mikoba ya Arthur Zwane. Pande hizo mbili ziko bize kupeana masharti ya kibinafsi kwa sasa.
Nasradinne Nabi ameiongoza Yanga kutwaa mataji mawili Yanga pamoja na Ngao ya jamii huku pia wakifika fainali ya kombe la shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya USM.
Ofa inayotamkwa zaidi ni ile ya Kaizer Chiefs ambao ndio kwa kiasi kikubwa wanahusishwa na Mtunisia huyo. Na walio karibu naye wanasema ana hamu ya kuchukua changamoto ya DStv Premiership.
Bosi wake wa Yanga Rais Hersi Said amevunja ukimya akitarajia kumpoteza kocha wake. “Ni wazi tumejenga kitu cha ajabu na kocha Nabi katika miaka miwili na nusu iliyopita,” Mhandisi Hersi aliiambia FARPPost. “Yupo kwenye klabu ambayo tumemuwekea mazingira mazuri ya kufanikiwa na amefanya vizuri.
“Ikizingatiwa mafanikio yetu kama klabu katika miaka miwili iliyopita, haishangazi kwamba vilabu vitavutiwa naye. “Tumekuwa na ratiba ya mechi nyingi katika msimu huu ambapo tumecheza michezo 55. Kwa hivyo mkataba mpya wa kocha haujajadiliwa ingawa tumefanya nia yetu ya kumuongezea.
Kocha Nabi inatajwa kuwa amewekewa takribani milioni 100 kama mshahara wake wa mwezi endapo atajiunga na wababe hao wa Afrika Kusini wanaotaka kurudisha ufalme wao mbele ya Mamelodi Sundowns.
Inaelezwa pia kama Nabi ataondoka Yanga basi huenda akaambatana na benchi lake la ufundi analofanya nalo kazi Yanga kwasasa na walilopata wote mafanikio msimu huu.
Mhandisi Hersi alizidi kufichua kuwa watamshirikisha kocha huyo kuhusu mustakabali wake na klabu hiyo kwa kuwa msimu umekwisha. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 amewahi kufundisha pia katika nchini za Libya, Sudan na Misri.