Sambaza....

Kiungo wa timu ya Vissel Kobe ya Japan Andres Iniesta amemshukuru na kumtakia kheri mchezaji Xavier Hernández Creus ‘Xavi’ ambaye ametangaza kustaafu kucheza soka la kulipwa mwishoni mwa msimu huu.

Iniesta ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa anajivunia kukua na kucheza pamoja na kiungo Xavi katika timu ya Taifa ya Uhispania na timu ya Barcelona na kwamba anamtakia kile lenye kheri katika maisha yake mapya baada ya kustaafu kucheza soka.

“Ni rafiki bora, nina heshima kubwa kukua pamoja nawe na kuwa pamoja nawe katika maisha yangu ya soka na kila kizuri tulichofanya pamoja, wewe ni mfano wa mchezaji bora, nashukuru kwa kila kitu zaidi kwa vile ulivyonifunza katika ulimwengu wa soka, nakutakia kila la kheri kwenye maisha yako mengine Xavi,” ameandika kwenye ukurasa wake.

Xavi mwenye umri wa miaka 39 ametangaza kustaafu soka akiwa na timu ya Al Sadd SC ya nchini Qatar ambayo alijiunga nayo mwaka 2015 akitokea Barcelona katika mipango ya kumalizia soka lake.

Mshindi huyo wa kombe la dunia la mwaka 2010 anastaafu akiwa ameichezea Barcelona kwa mafanikio makubwa akiichezea michezo 505 na kufunga mabao 58 huku akinyakua mataji lukuki ikiwemo mara nne taji la ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji nane ya La Liga.

Miongoni mwa mipango yake baada ya kustaafu ni kuingia moja kwa moja kwenye mipango an shirikisho la soka nchini Qatar katika kusaidia kuinua mchezo huo ili waweze kufanya vizuri kwenye michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2022.

Sambaza....