Upo usemi wa kale usemao “kijiji hakikosi wazee”, kijiji kikikosa wazee basi mambo mengi yataharibika. Wazee husifika kuwa na busara nyingi na uzoefu mkubwa katika kuyakabili mambo mbalimbali.
Kama kilivyo kijiji na wazee basi soka lina magwiji. Tunao magwiji maarufu wa soka duniani kama vile marehemu pele na Maradona, tunae Zinedin Zidane “Zizou”, Mtukutu Gatusso, Zlatan Ibrahimovic na wengine kibao.
Magwiji wamekua wakiendelea kutumika na vilabu na mataifa yao hata baada ya kutundika daruga, wanapewa ile thamani na nafasi kwa kuutambua mchango wao mfano wengine huwepo na kubaki kama viongozi klabuni na hata katika timu za mataifa yao.
Soka la Ulaya pengine ndio soka liliofanikiwa zaidi ulimwenguni kwani hupokea wachezaji kutoka karibia mataifa yote ulimwenguni, vilabu vimekua na utaratibu mzuri wa kuendelea kuwa karibu na wachezaji wao hata baada ya kustaafu na wengine wanaendelea kutumika hata katika ngazi za juu kabisa za uongozi wa vilabu mfano pale Bayern Munchen alikuwepo Olivier Khan kama mtendaji mkuu (CEO) alikuwa kipa wa zamani wa timu hiyo, pale Ac Milan alikuwepo Paolo Maladini kitasa cha boli hiki akiwa kama mkurugenzi wa ufundi, aliendelea kuhudumu hata baada ya kustaafu, pale Barecelona yupo Xavi Hernandez ni kocha mkuu wa Fc Barcelona, pale Arsenal yupo super Michael Arteta anahudumu kama kocha wa washika mitutu hao wa London na wengine wengi wanaendelea kuzitumikia timu zao. Ni utaratibu mzuri sana ambao timu na vilabu vya ulaya vimejiwekea.
Lakini hapa wetu Tanzania stori ni tofauti, nafasi ni finyu sana kwa magwiji kuendelea kutumika na timu zao hata baada ya kustaafu, maisha ya magwiji wa soka letu wanaishi maisha duni hakuna msaada wa moja kwa moja wanaoupata kutoka katika vilabu vyao wengine wamekua masikini wa kutupwa, wamevitumikia vilabu vyao kwa uaminifu na moyo lakini vilabu haviwapi thamani, sio tu vilabu hata nafasi katika timu zetu za taifa na hata nafasi za uongozi katika shirikisho la soka bado ni ndogo.
Kipi kinafanya magwiji wa soka letu wasithaminike na kupewa nafasi? Nini kifanyike?
• Ukosefu wa utaratibu mzuri wa kuwafuatilia wachezaji wao hata baada ya kustaafu soka ili kujua mienendo ya maisha yao ili kuweza kuwasaidia wanapokuwa katika nyakati ngumu, Hii itasaidia kunyanyua hali na morali ya kukubali kutumika tena na kuwa karibu na vilabu vyao, utaratibu mbovu iliopo sasa unawatenga mbali magwiji na vilabu vyao.
Hivyo vilabu vyetu na hata Taifa waanzishe utaratibu wa kuwasajili magwiji katika daftari la kudumu na kuwafuatilia kama fadhila ya kuthamini mchango wao.
• Ukosefu wa elimu; Ipo ile kasumba ya kuwa asilimia kubwa ya wanasoka hawana elimu ( hawakwenda shule) japokuwa wapo baadhi wana elimu ya juu sana lakini kasumba hii imewameza na hili limekuwa kama Zimwi linalowatafuna magwiji kiasi cha kutopewa nafasi kutokana na Elimu ndogo walizonazo.
Rai yangu kwa vilabu na Taifa, kuwekwe utaratibu mzuri wa kuwabaikiza magwiji wao na kuwapeleka shule(Darasani)ili wakapate elimu waje kuzitumikia tena timu zao mfano kuwapeleka kozi za uongozi na utawala na zile hata ukocha ili kuja kusaidia vilabu vyao na taifa kwa ujumla.
NB: Ukitaka kujua mwendo wa mjinga, mpe kiremba.