Moja ya maswali ambayo hadi sasa siwezi kutumia nguvu nyingi kuyajibu ni pale nitakapo ulizwa viungo wakabaji wa muda wote nchini Tanzania.
Nitawataja Chuji, Boban, Humoud, na Jonas Mkude kwa tafsiri ya haraka kwa majina hayo utajua ni sifa gani binafsi nazihitaji kwa kiungo wa dimba la chini.
Siku chache zilizopita (tarehe 29/08/2020) mtaalamu wa soka Athuman Idd Chuji ametangaza rasmi kustafu kucheza soka la kiushindani.
Polisi Dodoma, Simba, Yanga, Oman club, Mwadui, Coastal Union, Azam, na Singida United ni kati ya vilabu ambavyo vilifaidi matunda ya miguu na akili ya gwiji huyo.
Katika Chuji mmoja ulikua unaweza kupata viungo watatu kwa maana ya kiungo wa ulinzi, kiungo mchezeshaji na kiungo mshambuliaji, jamaa soka alilijua na lenyewe likamjua.
Viwanja vitafurahi kuondoka kwa miguu ya chuji, miguu iliyojaa uzito, nguvu na uwezo, nyasi zilikanyagwa na kuumizwa na miguu hiyo.
Mipira italia kuondoka kwa Chuji, itakumbuka mapenzi ya dhati toka kwake, itakumbuka namna aliichezea kwa mahaba na ufundi mkubwa.
Mashabiki watamkumbuka mwanaume huyu aliyefanya kazi kiume, mwanaume aliyeogopwa na timu pinzani na kuimbwa na timu yake.
Tanzania ‘taifa’ itamkumbuka chuji kwa mengi pasi kusahau mchango wake kwenye timu za taifa kuanzia alivyokua chini ya miaka 17 mpaka timu ya wakubwa.
Miaka 17 aliyohudumu katika soka kama mchezaji itakumbukwa na wadau wote wa soka na imani yetu kubwa ni kwamba bado tupo naye kwenye soka la nchi hii.
Amestaafu uchezaji lakini bado anaweza kuwa mwalimu, mshauri, kiongozi na hata mdau wa soka hili.
Kila lakheri kwako kiungo Athumani Idd Chuji katika mwanzo wa maisha yako mapya.