Sambaza....

Kocha Zahera Mwinyi alifanya mabadiliko mawili ya haraka haraka ndani ya dakika tatu na kuamua kutumia washambuliaji wane- wawili asilia na wawili wenye uifahamu wa kuzunguka eneo lote la mashambulizi.

Wala hakuogopa mashambulizi kadhaa mazito yaliyofanywa na KMC FC wakati, Mcongo huyo alipoamua kuwapumzisha viungo Mzimbabwe, Thaban Kamusoko dakika ya 74 na Rafael Daud dakika ya 77 na kuwapa nafasi mshambulizi, Mrundi, Amis Tambwe aliyeinga kuchukua nafasi ya Thaban na ‘yosso’ Maka Edward ambaye alichukua nafasi ya Daud.

Awali, dakika ya 63 kocha huyo wa Yanga alimtoa kiungo-mshambulizi wa pembeni Deus Kaseke na kumpa nafasi Matheo Anthony. Yalikuwa mabadiliko yaliyoendana na mahitaji na ushindi wa 1-0 ambao mabingwa hao mara 27 wa kihistoria Tanzania Bara wameupata Alhamis hii dhidi ya KMC FC umethihirisha wazi kuwa Zahera na mbinu zake yupo tayari kuipitisha Yanga katikati ya mabingwa watetezi Simba SC na mabingwa mara moja wa kihistoria- Azam FC ambao wamejidhatiti mno msimu huu chini ya kocha mshindi mara mbili wa ligi kuu Bara, Mholland, Hans van der Pluijm- Yanga inaweza kushinda taji hili sasa, hapana shaka.

Kumekuwa na fikra tofauti kuhusu mwenendo wa Yanga msimu huu- licha ya jana kufanikiwa kupata ushindi wa saba katika michezo nane, wapo wanaoibeza Yanga kwa kusema eti itapata wakati mgumu watakapotoka nje ya Dar es Salaam. Yanga itacheza na Lipuli FC siku ya Jumanne ijayo na mchezo huo utakuwa ni tisa mfululizo ‘Timu hiyo ya Wananchi’ itacheza katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ndiyo, lakini ni katika uwanja huo ambako wakiwa wageni waliweza kupata alama moja dhidi ya mahasimu wao Simba, na sasa wameifunga KMC katika namna ya kuvutia baada ya kupambana na timu bora kwa muda wote wa dakika 90’.

Kupata alama nne dhidi ya Simba na KMC ni ishara njema kuwa Yanga wanaweza kupata alama moja au tatu katika mchezo wao wa kwanza nje ya Dar es Salaam, Novemba 25 katika uwanja wa Kaitaba, Bukoba vs Kagera Sugar FC. Kukusanya alama zote 18 bila kuangusha yoyote katika michezo yao sita waliyokuwa wenyeji ni mtaji mkubwa sana kwa Yanga hivyo wanaweza kwenda ugenini wakiwa na mikakati na wakati huu klabu nyingi zikiangaika kunoa safu zao za mashambulizi na namna ukuta na safu za kiungo na mashambulizi zilivyo bila shaka mbinu za Zahera zinaweza kuanza safari za mikoani kwa mkakati wa ‘0-1=Pointi tatu muhimu au 0-0’ Yanga wanaweza kwenda mikoani na kuondoka bila nyavu zake kusumbuliwa kwa maana timu kama Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar FC, Mwadui FC, Lipuli FC, Coastal Union, Biashara United FC, Alliance School hazina uwezo mkubwa katika ufungaji .

Kusubiri Yanga waanguke mikoani kwa aina ya timu yao ya sasa inavyoendeshwa na mbinu za Zahera na kubeza matokeo ya jitihada zao jijini Dar ni ‘ujiinga’ ambao unapaswa kutoka kichwani na katika fikra za watu wanaoamini hivyo na wanaweza kurudia mchezo wa KMC 0-1 Yanga na kuona ni kiasi gani vijana wa Mcongo huyo wanavyoweza kushinda ubingwa msimu huu.

Kwanza usisahau kwamba timu hii ya Yanga imesainiwa kiufundi na asilimia kubwa ya wachezaji waliopo kikosini mwao wamesainiwa na makocha. Yanga bado wanakosa nguvu katika ukabaji lakini taratibu wameanza kuimarika katika ustahimilivu huku upambanaji wao ukionyesha wapo tayari kupambana kuchukua pointi tatu hadi dakika ya mwisho.

Kiki ile ya faulo iliyopigwa kiufundi na kiungo Feisal Salum dakika ya 90 na kumfunga kipa aliyekuwa kikwazo kikubwa-nahodha wa KMC, Juma Kaseja ni dalili kuwa zipo mbinu nyingi za Yanga kupata ushindi mchezoni. Matheo alichezewa faulo nje ya eneo la hatari na utulivu ulionyeshwa na Feisal unadhihirisha kuwa timu hiyo inabebwa kimbinu na kocha wao huku maarifa ya wachezaji yakichangia kusaidia kupatikana kwa ushindi.

Amini, Yanga hii ni tishio kubwa katika mbio za ubingwa msimu huu. Azam FC ilishinda 0-1 ugenini dhidi ya timu ngumu ya JKT Tanzania licha ya kucheza punguzu kwa zaidi ya daKika 65, Simba ilishinda 5-1 dhidi ya Alliance School na Yanga wameshinda 0-1 dhidi ya KMC- Ni ishara kwamba sasa ligi inaanza kuchanganya.’

Sambaza....