Hii ni Goodbye story, ndiyo story pekee ambayo husababisha koo kukauka kila ninapoanza kuisimulia.Kitu pekee ninachoshukuru Mungu ni kuwa nimepata neno GOOD ndani ya neno GOODBYE.
Goodbye story huumiza kipindi ambacho hadithi inapokomea njiani baada ya kitabu cha hadithi kufungwa. Nilitamani sana hadithi yake niendelee kuisoma, hadithi ambayo ilianzishwa na neno pole. Lilikuwa neno la kikarimu lililotoka kwenye kinywa cha kijana mmoja mkarimu sana, neno ambalo lilienda sambamba na kuionea huruma mikono yangu iliyokuwa imebeba begi zito.
Huu ndiyo ulikuwa mwanzo wa kitu kipya kwenye maisha yangu, mwanzo ambao ulinipa nafasi kubwa ya mimi kuwa sehemu ya maisha yake. Kwangu mimi hakuwa binadamu pekee ila alikuwa nyumba ambayo nilistahili kuishi.
Alinifanya niwe mwanamke mwenye amani, alinipenda na alipokea upendo wangu. Hakutaka kuniona naishi kawaida, ndiyo maana alitumia muda mwingi kunisisitiza nisiwaze kuishi kawaida katika dunia ambayo siyo ya kawaida.
Upendo wake haukuwa wa kawaida. Kwa kifupi hakuwa mtu wa kawaida. Nakumbuka vitu vingi sana kutoka kwake. Nakumbuka siku ya kwanza alivyonishika mkono, siku ya kwanza alivyonitazama machoni na kuniambia kuwa ananipenda, ilikuwa siku ambayo dunia ilisimama kuzunguka katika mhimili wake na kubaki ikitutazama huku ikitabasamu, namkumbuka sana.
Nakumbuka nyakati ambazo nilikuwa na kata tamaa, ulimi wake ulitumika kama mkono kuniinua nilipokata tamaa. Nakikumbuka pia kipaji chake.
Mimi siyo mpenzi wa mpira wa miguu ila nilisikia Rafiki zake wakimwiita Ronaldinho Gaucho, nilipowauliza kwanini wanamwiita hivo waliniambia ni kwa sababu miguu yake imejaa sanaa ya kuuchezea mpira, kuna wakati walimwiita Ronaldo De Lima kwa sababu walimuona ni namba tisa bora, ufungaji wake wa magoli ulifanya marafiki wamwiite Cristiano Ronaldo. Mara nyingi rafiki zake walipenda kumwambia ana akili kubwa ya mpira ndiyo maana walipenda kumwiita Lionel Messi.
Alikuwa mchezaji aliyekamilika, kuna wakati nilitamani nione nchi yangu ikijivunia kipaji chake lakini leo hii naandika Goodbye story. Najihisi mtu mwenye bahati kupata mtu ambaye ananiwia vigumu kusema kwa heri. Hakuwahi kutamani kuishi milele ila alitamani kutengeneza kitu ambacho kingeishi milele.
Mwili wake ulikuwa Simiyu ila akili na matamanio yake yalikuwa kutaka kucheza RealMadrid ya Hispania.
Asubuhi na jioni alifanya mazoezi. Kitu pekee ambacho nilikiona kwake ni bidhaa. Nilimuona ni bidhaa, bidhaa ambayo ingeuzwa nje ya nchi na kuwa bidhaa pendwa kuzidi zote duniani.
Bidhaa ambayo sisi Watanzania tungejivunia kama tunavyojivunia kwa sasa kuwa na Mbwana Samatta. Kitu pekee kilichokosekana kwake ni kupata mfanyabiashara sahihi wa kuiuza bidhaa hiyo. Kila aliyebahatika kumtazama alibaki mdomo wazi kwa kipaji kile. Alisifiwa na kila mtu lakini alikosa wakala sahihi wa kumtoa Simiyu na kumpeleka sehemu sahihi.
Siku zilizidi kwenda, umri ukawa unahesabika kwa kasi, nguvu za miguu zikaanza kuisha taratibu. Ule ufundi aliokuwa nao ulianza kupungua taratibu, ndoto yake ya kucheza Ulaya ikaanza kutoweka taratibu, umri wa majukumu mengi ukaanza kumyemelea taratibu. Kuna wakati majukumu yalimzidi. Msongo wa mawazo ukamvaa kitu pekee alichokiona kinafaa kumuondolea msongo wa mawazo ni pombe. Akaanzisha rasmi urafiki na pombe, kila muda alitembea na pombe. Ulevi uliruhusu ngono zembe kitu kilichopelekea yeye kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Leo hatuko nae tena., wimbo wake umeisha lakini melody ya wimbo wake bado ipo kichwani mwangu. Goodbye Samatta, Ronaldo wetu wetu. Nilikuwa sifahamu kuwa neno GOODBYE linaambatana na maumivu.Nina bahati nzuri sana kwa sababu nilipata mtu ambaye inaniwia vigumu kumwambia kwa heri.
Hata kama sikuishi naye muda mrefu ila nashukuru alikuwa sehemu ya maisha yangu. Asante. Asante kwa kuja kwenye maisha yangu na kunipa furaha. Asante kwa kunipenda na kupokea upendo wangu, asante kwa kumbukumbu. Kifo siyo mwisho ila ni mwanzo ni maisha mapya.
Maisha ambayo yatatengeneza mazingira bora ambayo yatahakikisha vipaji mbalimbali visipotee. Natamani maisha ambayo TFF itatengeneza ma scouts wengi ambao watazunguka kila kona ya nchi hii kutafuta vipaji vikubwa. Natamani maisha ambayo yatakuwa na mawakala wengi , vituo vingi vya kuibua, kulea na kukuza vipaji. Natamani kuona mazingira ambayo yanaonesha kuwa mpira ni biashara kubwa. Hii ni Goodbye story ya aliyewahi kuwa Samatta wangu.