Wananchi Yanga hatimae wanafanikiwa kuandika historia si tu ya klabu yao lakini pia kwa Afrika nzima baada ya kuibuka na ushindi mbele ya Marumo Gallants na kufanikiwa kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya ushindi wa mabao mawili kwa bila katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali wakiwa nyumbani na ushindi wa mabao mawili kwa moja unaifanya Yanga kufuzu kwenda fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao manne kwa moja dhidi ya Marumo Gallants.
Katika mchezo wapili uliopigwa katika Dimba la Royal Bafokeng na Yanga kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja, magoli ya Yanga yalifungwa na Fiston Mayele katika dakika ya 45 kipindi cha kwanza na bao lapili likifungwa na Kennedy Musonda katika dakika ya 69 ya mchezo na hivyo kuihakikishia safari ya fainali Yanga.
Sasa Yanga wanasubiri mshindi kati ya Asec Mimosa ama USM Algier ambao katika mchezo wakwanza Asec akiwa ugenini ulimalizika na suluhu na hivyo USM Algier kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwafwata Wananchi katika mchezo wa fainali.
Michezo ya fainali itapiwa May 28 na ule wa marudiano ni June 03 mwaka huu ambapo kama kawaida fainali hizo zitapigwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na si kama msimu uliomalizika ambapo ulipigwa mchezo mmoja pekee.
Kwa ushindi huo sasa Yanga wanakua timu ya pili ya Tanzania kucheza fainali za michuano ya Afrika na kufikia rekodi ya Simba ambao walicheza fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 walicheza fainali dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Lakini pia ndio timu pekee kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) iliyofika mbali na kufanya vyema katika michuano hiyo yapili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu msimu huu.
Yanga haikufika fainali kwa bahati mbaya ama kwa wasiwasi kwani katika michezo yote ya Kombe la Shirikisho msimu huu wamepoteza mchezo mmoja pekee tena katika hatua ya makundi wakiwa ugenini dhidi ya US Monastir ya Tunisia.