Kama utani tu Beatrice Ndugu ameamua kumfanya Haji Manara kuwa bidhaa yenye thamani kubwa hapa nchini. Bidhaa inayouzika, bidhaa ambayo watu wengi watatamani kuitumia kwa kutoa pesa zao mfukoni na kumkabidhi Haji Manara.
Haya yote ni kwa sababu moja tu , nayo ni KIPAJI. Kipaji cha Haji Manara ndicho kinachofanywa biashara na mwanadada mrembo Beatrice Ndugu. Wakati sisi kila uchwao tunatamani kumsikia Haji Manara amesema nini, Beatrice Ndugu yeye anafikiria atafanya nini kutokana na kipaji cha Haji Manara.
Kipaji cha kuongea, huyu ni mwanadamu aliyekuja dunia kwa kazi moja tu kubwa ya kumwingizia kipato, nayo ni kuongea. Furaha ya Haji Manara ipo kwenye kuongea, anaweza akaumwa wiki nzima kama utamnyima nafasi ya kuongea ndani ya saa moja tu.
Yeye kila mara mdomo wake unawasha, lips zake zinatamani kutanuka kila mara. Ni ngumu yeye kutulia hata siku moja. Leo ataongea Yanga kiutani. Siku itaenda, kesho ataiongea klabu yake Simba kwa wema siku itapita vizuri tu. Kesho kutwa utamkuta anazungumza kuhusu masuala ya udaku. Tena ataongea kwa ustadi mkubwa sana kuhusu udaku. Hata kumsifia mwanamke mzuri kwake ni jambo jepesi sana na analifanya kwa ustadi mkubwa. Ushawahi kumsikia akimuongelea Dada yangu Jokate ?
Hapana shaka utagundua yeye ni mwanadamu ambaye kipawa cha kuongea ni miliki yake kubwa, ndiyo maana hata siasa yeye anaongea tu.Mwisho wa siku ana pata nini ?, utakuta Haji Manara ana mashabiki wengi kwenye kona nyingi za maisha ya kawaida ya mwanadamu.
Shabiki wa udaku utamkuta anamfuata Haji Manara kwenye mitandao ya kijamii, shabiki wa siasa, wa mpira.Mwisho wa siku Haji Manara anajikuta anakila aina ya watu wanaomfuata. Waheshimiwa watamfuata kwa sababu ya mpira na siasa.
Ndiyo maana kwenye tangazo lake la siku ya kuzaliwa kwake ambayo ataitumia kama siku ya kuzindua manukato yake kuna sura ya watu wenye hadhi kubwa hapa nchini.Hawa ni mashabiki wake, ndiyo maana walipoarikwa kuudhulia hafla hii hawakuweza kujiuliza mara mbili mbili, walikubali.
Yote haya yanafanyika kwa sababu kuna mtu ambaye ni muhimu sana kwa Haji Manara kwa sasa. Mtu ambaye hata wengi hamtujui sana.
Beatrice Ndugu , huyu ndiye mwanamama anayepanga kila kitu hiki kionekane kama kilivyo kwa sasa.Huyu ndiye anayemfanya Haji Manara awe na mashabiki wa kila aina. Huyu ndiye anayemuongoza Haji Manara aonekane kuwa nembo ya biashara.
Huyu ndiye anayemfanya Haji Manara auzike vizuri kwenye macho ya wengi, na huyu ndiye anayetuletea manukato ya Haji Manara.Tutayatumia sana , tutayanunua sana na mwisho wa siku Haji Manara atanufaika sana na kipaji chake kutokana na pesa ambazo ataingiza.
Haji Manara aliona hatoweza kufanya yote haya kwa kutumia nguvu na akili zake pekee. Ndiyo maana akamtafuta Beatrice Ndugu.Alimwajiri kuwa Brand Manager wake. Huyu ndiye anayeshughulika na namna ya kuiuza nembo ya Haji Manara nje. Nembo yenye mashabiki wengi sana.
Nembo ambayo kuna watu wengi wanayo lakini hawajui jinsi ya kuitumia iwe biashara nzuri kwao hata siku moja.Moja ya watu ambao wanaweza kutumika kama nembo kubwa kibiashara ni wachezaji wetu ambao moja ya viongozi wao ni hawa kina Haji Manara.
Hawa ndiyo wanaotusababisha sisi twende uwanjani, hawa ndiyo wanaotusababisha sisi tufurahie na wakati mwingine kuhuzunika.Macho yetu yako kwao kwa kiasi kikubwa. Kuwafuatilia wao , kwao wao ni biashara lakini wanakosekana watu kama kina Beatrice Ndugu kwao wa kuwaamsha.
Wengi wamelala, tena usingizi wa pono. Hawajitambui kabisa kwa bahati mbaya. Wamekosekana wasimamizi sahihi wa kuwatoa kwenye usingizi.Wasimamizi ambao watawaonesha namna nzuri ya kutumia mitandao ya kijamii kujikuza kibiashara. Wasimamizi ambao watawafanya wachezaji wawe nembo ya kibiashara nje ya uwanja.
Wachezaji wetu hawafikiri kabisa kuwa na wasimamizi wa vipaji vyao, kuna wakati nafikiria huwa hawaumii kusikia habari kama hizi za kina Haji Manara?Hawaumia kuona Haji Manara anakiuza kipaji chake?, hebu waumizwe na hii hali kisha watafute wasimamizi wazuri wa vipaji vyao.