Sambaza....

JANA jioni Zanzibar Heroes wamekufa kiume katika ardhi ya Mzee Jomo Kenyata pale Kenya. Wamekufa kiume kwa mapigo ya penati. Mapigo ya penati hayajawahi kuwa na mwenyewe. Well done boys. Well done coach Moroco.

Ndani ya mchezo ule Moroco na vijana wake wametuonyesha kwanini mchezaji wa timu ya taifa anajisikia fahari kuivaa jezi ya taifa lake na kulitumikia kwa asilimia 100.

Heroes walijitoa sana uwanjani. Walicheza katika pumzi yao ya mwisho. Walipambana kama hawachezi tena mechi nyingine na jana ndiyo walikuwa wakicheza mechi yao ya mwisho. Aina ya mchezo wao ilitupa neno sahihi la mechi ya machozi, jasho na damu.

 

Kuanzia benchi lao, hadi uwanjani kila mmoja alimuhimiza mwenzie. Zamani kidogo kuiona timu ya Tanzania Bara ikicheza hivi. Kuna kitu wametufundisha sisi watu wa Bara tunaowapenda wachezaji wetu wanaouza sura katika kurasa za mbele za magazeti ya michezo kila uchwao.

Wakati mwingine huitaji utalamu ili kushinda mechi, unahitaji jeshi la wanaume 11 na wengine saba wanaokaa benchi kumsikiliza mwalimu na kufuata maagizo yake. Full stop.

Katika kikosi cha Kili Stars kilichoenda Kenya ni Himid Mao pekee anayeweza kucheza katika mizani ya wachezaji wa Heroes, wengine wote walienda Kenya kutuibia. Nisameheni rafiki zangu. Leo nimeamua kumtafuna jongoo. Sina namna nyingine. Naomba mnisamehe!

Kando ya matatizo makubwa yanayolikumba soka la Tanzania kiujumla, lakini wachezaji wa Bara walukosa kujitoa uwanjani kututetea sisi tulioko nje ya uwanja. Walicheza kwa kujisikia mno.

Kilichowafikisha Heroes pale walipofika na leo kupokewa kishujaa ni kujitoa kwao na kujua uzito wa jezi walizovaa. Sisi Bara tumekosa hii spirit.

Ukiachana na umahiri mkubwa wa kichezaji walionao wachezaji wao wengi, lakini nyuma yake wanasukumwa na kujitoa. Sehemu ya kutia mguu, wanatia mguu kweli, sehemu ya kutia kichwa wanatia kichwa kweli. Siku ambayo wachezaji wa Bara wataamua kujitoa kama walivyojitoa Heroes, kuna hatua tutapiga.

Heroes ya jana ilinikumbusha Mbeya City ‘dume’ ileeee, sio hii ya sasa inayofungwa 5-0 na wachezaji wake wanatoka uwanjani wanachukulia poa na mwisho wanaomba selfie.

Feisal Salum Abdallah (Fei Toto ). Mmoja ya viungo wa Heroes anayekupa radha ya Gennaro Gattuso na wakati huo huo akikupa radha ya Andres Iniesta. Huyu ndiyo amewahamisha Mudathir Yahya na Banka Koke(Mohamed Issa) wacheze pembeni kati wamuache yeye na Abdulaziz Makame ( Bui).

Heroes ni hatari. Wanavutia kuwatazama. Ndani ya uwanja hawaishii kukupa sex football, wanakupa na spirit ambayo haipatikani kwa rafiki zangu wengi. Leo nisameheni.

Stars yetu imejaza kundi kubwa la wachezaji wanaocheza na ‘vioo uwanjani’ kwa ajili ya kujitazama. Hawaoni uzito wa jezi wanaovaa wala kuhurumia makundi ya mashabiki wanaomwaga povu hivi sasa. Masikini Kili Stars yangu.

Siamini kama Bara inashindwa kuwa na mchezaji mwingine wa daraja la Mbwana Samatta. Naamini wako wengi sana. Hadi mtaani pia wako, lakini wengi wao ni wale wavivu wa mazoezi, ujasiri na wamekosa uthubutu. Mbwana amewazidi wenzake vitu hivyo vitatu. Hajawazidi vitu vingine.

Jitihada za Heroes zichukuliwe kwa mtazamo hasi kwa rafiki zangu ambao ni mahiri wa kuvaa eraphone kubwa kubwa na kubeba lundo la viatu mikononi na kichwani wakibadili mitindo ya nywele kama wanavyobadili nguo zao za ndani.

Ingekuwa sijatenda haki kama andiko hili lingeenda hewani bila kutaja jina la mwanaume mmoja wa shoka anayeitwa Ibrahim Hamad Ahmada. Jamaa ni bonge la mchezaji. Anacheza kwa uchungu, anahamasisha kwa uchungu na anashangilia kwa uchungu. Anaonekana anafurahia kuwatumikia Wazanzibar. Mzaramo kanena Zuwa Diswa.

Sambaza....