Sambaza....

Beki wa zamani wa klabu ya Yanga Hassan Kessy ambaye kwa sasa ajamalizia msimu wake na timu ya Nkana FC ya Zambia anaweza akarejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga.

Hassan Kessy ameutaarifu mtandao huu kuwa kwa sasa anachosubiri tu mkataba wake uishe ili aone sehemu gani sahihi ambayo ataenda baada ya kuitumikia Nkana FC ya Zambia.

“Kwa sasa bado nina mkataba na Nkana FC na nina subiri mkataba wangu uishe ili nione ni wapi naweza kwenda, kama ni kuongeza mkataba au kwenda timu nyingine tutajua baada ya mkataba wangu na Nkana FC kuisha”- alisema beki huyu mahiri wa kushoto.

Beki huyo alisisitiza pia kuwa anatamani kuendelea kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kama ambavyo kwa sasa anavyocheza nchini Zambia katika klabu ya Nkana FC , klabu ambayo imemwezesha kucheza michuano ya CAF.

“Kwa sasa bado natamani kucheza katika ligi ya kulipwa zaidi. Natamani kucheza nje ya nchi kwenye soka la kulipwa zaidi”- alisema Hassan Kessy.

Kuhusu yeye kurudi kwenye klabu ya Yanga, Hassan Kessy amedai kuwa uwezekano upo kama kutakuwepo na mazungumzo pande zote mbili yani upande wa Yanga na upande wa Hassan Kessy.

“Kama wataonesha nia ya kunihitaji , nitaongea nao na nitaona kama naweza kurudi kwenye klabu yangu ya zamani uzuri tuliachana nao vizuri , na nina uwezo wa kupigania namba pia”- alimalizia beki huyo wa timu ya taifa ya Tanzania .

Sambaza....