Baada ya kuanza vizuri kwenye kikosi cha Nkana FC mpaka kufanikiwa kabisa kupenyeza katika kikosi cha kwanza cha Nkana FC mambo yameanza kwenda vibaya kwa beki mahiri wa kulia wa Tanzania , Hassan Kessy.
Hassan Kessy kwa sasa amekuwa akihangaika kupata nafasi ya kikosi cha kwanza kama ambavyo alivyokuwa anapata awali kutokana na kinachosemekana kushuka kiwango.
Akizungumza akiwa Nairobi , safarini kuelekea Zambia Hassan Kessy amedai kuwa mpaka sasa hivi ana mkataba na klabu hiyo ya Zambia na wakala wake yuko Zambia kwa mazungumzo zaidi.
“Mpaka sasa hivi nina mkataba na Nkana FC, wakala wangu yuko Zambia kwa ajili ya kuliongelea hili suala” alisema beki huyo mwenye uwezo wa kupanda na kushuka.
Alipoulizwa kuhusu yeye kufukuzwa kwenye kikosi hicho alidai kuwa hicho ni kitu cha kawaida kwenye mpira.
“Hiki ni kitu cha kawaida kwenye mpira hata Ulaya hutokea , ila kwa sasa Mimi nipo na Nkana nina mkataba na Nkana” alimalizia mchezaji huyo. Hassan Kessy kabla ya kwenda Nkana FC alikuwa mchezaji wa Yanga.